Johato arejerewa mwanae aliepokwa na ndugu wa Baba aliezaa nae

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 07:26 PM Jul 13 2025
news
Picha Mtandao
Ofisa wa Wizara ya Sheria akitoa maelezo kwa Mama aliekuwa na uhitaji wa msaada wa kisheria, picha haihusiani na stori.

MAMA aliyenyang'anywa mtoto wake kwa miezi sita, amerejeshewa baada ya kusaidiwa na Wizara ya Katiba na Sheria kupitia Kampeni ya Kisheria ya Mama Samia, kwenye viwanja vya maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (DITF).

Mama huyo Johato Ally, alifika juzi katika banda hilo la Katiba na Sheria na kuomba asaidiwe na baada ya kusikilizwa na jopo la Maofisa wa Sheria wa Wizara kupitia Kampeni hiyo ya Kisheria ya Mama Samia, waliopo katika maonesho hayo waliamuru mama huyo arejeshewe mtoto wake huyo mwenye umri wa miaka miwili. 

Kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Wizara imefanikiwa kurejesha tabasamu kwa Johari Ally ambaye alikua amenyang’anywa mtoto wake wa miaka miwili na ndugu wa Baba aliyezaa naye. 

Julai 10,2025 Johari alifika katika banda la Wizara ya Katiba na Sheria akiwa anahitaji msaada wa kisheria wa namna ya kumpata mwanae aliyechukuliwa na ndugu wa Baba yake kwa takribani miezi sita.

Mama huyo alinyang'anywa mwanae na ndugu wa mwanaume aliyezaa naye.

Baada ya kumsikiliza mama huyo, jopo hilo la wanasheria liliamuru ndugu waolinyang'anya mtoto huyo wafike katika viwanja hivyo siku iliyofuata na juzi wakafanikiwa kuwakutanisha na baada ya mazungumzo ndipo mama huyo alirejeshewa mwanaye.

Jopo hilo liliwashauri ndugu hao kwamba pale watakapokuwa wakimhitaji mtoto huyo kumsalimia wakubaliane na mama huyo.

Akizungumza baada ya kufanikiwa kumrejesha mtoto kwa mama yake, Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Haki za Binadamu, Beatrice Mpembo alisema kuwa haikua rahisi kufanikisha jambo hilo.

"Changamoto zilikuwa kubwa, lakini tulipambana sana kisheria mpaka tukafanikisha kwa sababu sheria za nchi zinataka mtoto wa umri huo akae na mama yake, jambo la kushukuru ni kwamba tulilimaliza kwa amani," alisema Beatrice.

Akizungumza baada ya kukaidhiwa mwanae, Johari alitoa shukrani kwa Serikali na Wizara ya Katiba na Sheria kwa kuendesha Kampeni ya Msaada wa Kisheria iliyomsaidia kumrejesha mwanae kwake. 

Wizara ya Katiba na Sheria ilishiriki katika maonesho hayo ya 49 ya DITF, kutoa huduma za msaada wa kisheria pamoja na elimu ya sheria.

Kwa mujibu wa Beatrice, baada ya muda wa maonyesho kuisha wananchi wote wenye changamoto watawasilisha migogoro yao  Wizarani pamoja na  kupitia kituo cha Huduma kwa Mteja kwa namba 0262160360.