Majaliwa aiagiza Tantrade kufanya utafiti masoko ya ndani

By Elizabeth Zaya , Nipashe
Published at 10:57 AM Jul 14 2025
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa
Picha: Mpigapicha Wetu
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameiagiza Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) kuendeleza juhudi za kutafuta masoko ya nje ili kuongeza mauzo yatakayowezesha nchi kupata fedha za kigeni.

Amesema kuwa TanTrade inapaswa kufanya tafiti za uhakika na uchambuzi wa masoko ambayo bidhaa za Tanzania zinaweza kuuzwa na kutoa taarifa hizo kwa wafanyabiashara kote nchini.
 
Ametoa agizo hilo katika ufungaji wa Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar-es-Salaam(DITF) yaliyohitimishwa jana.
 
“Masoko yamekuwa ya ushindani sana siku hizi, nilipotaja Soko Huru la Biashara la Afrika (AfCFTA), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) nilikuwa nataka kuwaambia kwamba leo hii tunapotaka kufanya uchambuzi wa masoko yetu, hayo ndio maeneo ya kufanya biashara, TanTrade fanyeni tafiti za uhakika na uchambuzi wa kina,"amesema Majaliwa.
 
Kadhalika, ametoa wito kwa wazalishaji wote nchini kuweka mkakati wa kuongeza uwekezaji na uzalishaji wa bidhaa ambazo zina mahitaji makubwa katika masoko ndani na nje ya nchi.

“Maonesho haya ya 49 ya biashara yanapaswa kuwapa mwanga wa bidhaa gani zina mahitaji makubwa ili muongeze uzalishaji, tunahitaji kupanua wigo wa masoko kwenye mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi."
 
Amewataka wazalishaji hao, kuzalisha bidhaa zenye ubora mkubwa ili watumiaji waridhike na ubora wake na zimudu ushindani wa kimataifa. 

Amewaagiza kutumia nembo ya  Made in Tanzania katika bidhaa zao zote.
 
Majaliwa amezitaka taasisi zote zinazosimamia Biashara na Uwekezaji, Tanzania Bara na Zanzibar, zihakikishe zinaondoa urasimu na kuwezesha Biashara zaidi badala ya kuwa kikwazo.
 
Amesema serikali ya itaendelea kuhamasisha biashara na uwekezaji zaidi katika maeneo ya kimkakati ili kuchangia kikamilifu katika pato la taifa na kunufaisha wananchi.
 
Waziri wa Viwanda na Biashara Dk. Selemani Jafo, amesema katika kipindi cha siku 16 za maonesho hayo, watu zaidi ya milioni 2.4 wameshiriki katika shughuli mbalimbali za maonesho hayo ya kimaitaifa ya biashara.