Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amemwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan katika Mkutano wa Saba (7) wa Uratibu kati ya Umoja wa Afrika na Jumuiya za Kikanda uliofanyika jijini Malabo, Equatorial Guinea.
Rais wa Jamhuri ya Equatorial Guinea, Teodoro Mbasogo amefungua mkutano huo na kusisitiza mtangamano wa Afrika na utekelezaji wa Mkataba wa eneo huru la biashara inayolandana na jukumu la Mkutano wa Uratibu la kutambua maeneo ya ushirikiano na kuanzisha mifumo ya ushirikiano ya kikanda na kimataifa katika kuendeleza juhudi za kukuza uchumi wa nchi wanachama.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU, Mahmoud Ali Youssouf amezisisitiza nchi wanachama kuzipitia na kuzifanyia mabadiliko sheria za kodi za nchi zao Ili kuongeza mapato ya nchi wanachama.
Naye Mwenyekiti wa AU na Rais wa Jamhuri ya Angola, João Lourenço katika hotuba yake amewekea mkazo wanachama kutatua migogoro yao wenyewe na kueleza kuwa pembezoni mwa kikao cha Umoja wa Mataifa kitakachofanyika mwezi Septemba, kitaitishwa kikao cha viongozi wa Afrika kujadili vyanzo vya migogoro Afrika na namna bora ya kuvikomesha. Pia amezitaka nchi za Afrika kuwekeza katika ubunifu wa kisayansi ili kuharakisha maendeleo Afrika.
Katika Mkutano huo ambao ndio jukwaa kuu la kuratibu utangamano wa kikanda, taarifa mbalimbali zimewasilishwa. Taarifa hizo ni pamoja na hali ya mtangamano wa kikanda na nafasi ya Shirika la Maendeleo Afrika katika Mtangamano wa Kikanda barani Afrika.
Nyingine ni Hali ya Mgawanyo wa Majukumu kati ya Nchi Wanachama, Umoja wa Afrika na Jumuiya za Kikanda, Kamisheni ya Umoja wa Afrika kuhusu Utekelezaji wa Kaulimbiu ya Mwaka 2025 ya Umoja wa Afrika na Uratibu na uoanishaji sera za Umoja wa Afrika/ Jumuiya za kiuchumi za Kikanda
Umoja wa Afrika una Jumuiya nane (8) za kikanda ambazo ni, UMA, COMESA, CEN-SAD, EAC, ECOWAS, ECCAS, IGAD na SADC.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED