Kampuni 15 za kimataifa zimeonesha nia ya kuwekeza katika Kongani Maalum ya Uwekezaji ya Buzwagi (SEZ) iliyopo mkoani Shinyanga, eneo ambalo awali lilikuwa Mgodi wa Dhahabu wa Buzwagi uliofungwa mwaka 2019.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma kupitia mpango wa Idara ya Habari (MAELEZO) wa kutangaza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita, Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Mboni Mhita, amesema kuwa kongani hiyo inalenga kufufua mzunguko wa fedha uliokuwepo wakati mgodi huo ukiwa hai.
“Wananchi watanufaika kwa kupata ajira, kuuza bidhaa na kushiriki katika mnyororo wa thamani. Zaidi ya hayo, Wilaya ya Kahama imepata ufadhili kutoka Benki ya Dunia (WB) kwa ajili ya ujenzi wa barabara za kiwango cha lami,” amesema.
Ameeleza kuwa kongani hiyo itakuwa ya kipekee kwa kuwa na miundombinu ya kisasa, ikiwemo kituo chake cha kuzalisha umeme kwa matumizi ya ndani ya eneo hilo.
“Hadi sasa, kampuni ya East Africa Conveyers Service tayari imeanza uzalishaji, wakati kampuni nyingine nne zipo katika hatua za awali za kupata leseni na zimeshafanya usajili wa miradi yao kupitia NEMC. Pia, Kampuni ya Kabanga Nickel tayari ipo ndani kule kwa ajili ya kuwekeza eneo hilo,” amesisitiza.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED