OFISA wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya, Selemani Mbwambo amedai wakati akishuhudia ufungaji wa kielelezo cha dawa za kulevya washtakiwa walikuwa watatu lakini mmoja alifariki akiwa gerezani.
Shahidi alidai hayo Mahakama Kuu Divisheni ya Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi mbele ya Jaji Godfrey Isaya wakati akitoa ushahidi kwa kuongozwa na Wakili wa Serikali Mwandamizi Mafuru Moses.
Alidai Juni 24 mwaka 2021 akiwa kazini alipangiwa kazi na kiongozi wake ya kushuhudia kielelezo kikifungwa kwa ajili ya kupeleka Mabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali kwa ajili ya uchunguzi.
Alidai alikwenda katika chumba cha kufungia vielelezo alimkuta Inspekta Johari akiwa na watu kadhaa, akatambulishwa kwa washtakiwa pamoja na shahidi huru.
"Washtakiwa walikuwa watatu, Saidi Rashidi Mgoha, George David Mwakang'ata na Andrew Paul, shahidi huru Fadhili Kitiku.
Alidai Inspekta Johari alitoa pakiti moja, aliikata ili kuona kilichomo ndani, waliona chenga chenga za rangi ya krimu zilizodhaniwa kuwa dawa za kulevya.
"Inspekta Johari aliwauliza watuhumiwa, kielelezo hiki ndicho mlichokutwa nacho, walisema ndio,"alidai.
Alidai kielelezo kilifungwa, watuhumiwa, shahidi huru pamoja na shahidi wote waliandika majina yao juu na kusaini.
Alidai ufungaji kielelezo ulikamilika, alichukua kielelezo akaenda kukihifadhi katika chumba cha kutunza vielelezo.
Alidai Juni 24 mwaka 2021 mchana alikabidhiwa bahasha yenye alama A2 juu ikiwa na majina ya watuhumiwa kwa ajili ya kupeleka kwa Mkemia Mkuu wa Serikali kwa uchunguzi.
Shahidi alidai alikabidhi bahasha hiyo mwa Mkemia Edward Dilunga ambaye aliisajili na kuipa namba LAB1915/2024.
Alidai Mkemia alipima uzito na kufanya uchunguzi wa awali ambapo alibaini chenga chenga zilikuwa dawa za kulevya aina ya heroine kilo 1.02.
Wakili Mafuru alitaka shahidi kuwatambua washtakiwa watatu aliowaona wakati kielelezo kinafungwa kama wapo mahakamani.
Shahidi alidai kizimbani anawaona washtakiwa wawili Saidi Rashidi na George David lakini Andrew Paul hamuoni, kwa taarifa alizosikia alifariki dunia akiwa gerezani.
Akihojiwa na Wakili wa utetezi, Josephat Mabula alidai hakuona umuhimu wa kuongozana na watuhumiwa kwenda kwa Mkemia kushuhudia uchunguzi kubaini chenga chenga kama dawa za kulevya ukifanyika.
Alidai kwa ufahamu wake mshtakiwa Paul alifariki Dunia na akitakiwa kuwasilisha ushahidi kuthibitisha ataleta.
"Taarifa nilizisikia kwamba Andrew kaaga Dunia , hapa sina ushahidi nilisikia kama ulivyosikia wewe, nikiambiwa nilete ushahidi nitaleta,"alidai shahidi.
Washtakiwa katika kesi hiyo wawa kuwa Juni 21 mwaka 2021 maeneo ya Mivinjeni Dar es Salaam walikamatwa wakisafirisha heroine kilo 1.02.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED