Cobra; Mkubwa zaidi mwenye sumu duniani

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 02:57 PM Jul 14 2025
Forest Cobra
Picha: Mpigapicha Wetu
Forest Cobra

KWENYE jamii kuna viumbe wanaoogopwa na kuonekana umuhimu wao ni mdogo. Dhana hiyo ipo kwa nyoka.

Anaogopwa na binadamu wengi. Wiki hii kuelekea kilele cha Siku ya Nyoka Duniani, Julai 16, 2025, Nipashe Digital, inakuletea mfululizo wa maelezo kuhusu nyoka. 

Mkufunzi kutoka Chuo cha Uhifadhi Wanyamapori cha Afrika Mweka, Tito Lanoy, alifafanua kuhusu historia na tabia zao, ikiwamo kujilinda kwa kutoa sumu au kutumia rangi yake, kuelekea kilele cha Siku ya Nyoka Duniani.

Lanoy, ambaye pia ni Mwanzilishi na Rais wa Tanzania Jamii ya Wataalamu wa Nyoka Tanzania, amesema nyoka ni miongoni mwa viumbe vya kale zaidi kwenye hadithi na tamaduni na vimetukuzwa na jamii mbalimbali duniani kote.

“Kufikia sasa, kuna aina takribani 4,038 za nyoka duniani, wanaopatikana kuanzia kwenye baridi kali ya kaskazini mwa Canada hadi kwenye misitu ya mvua ya maeneo ya Ikweta na hata kwenye bahari nyingi duniani.

“Kati ya aina hizo, nyoka 725 wana sumu na ni aina 250 tu wenye sumu kali inayoweza kuua binadamu,” amesema Lanoy.

Amesema nyoka ni wawindaji hodari sana na husaidia sana katika kuleta usawa wa mfumo wa ikolojia. 

“Cha kuvutia zaidi ni kuwa nyoka ni viumbe wa enzi za kale, na hutupatia mwanga juu ya maisha ya nyakati za kabla ya historia wakati ambao dunia ilitawaliwa na reptilia”.

Amewataja baadhi ya nyoka wanaovutia watu zaidi ambao ni King Cobra ambaye ni nyoka mkubwa zaidi mwenye sumu duniani, anayejulikana sana kupitia sinema.

Amemtaja mwingine kuwa ni Rattlesnake, anayejulikana kwa sumu yake kali kiasi kwamba watu hulazimika kunyonya sumu kutoka kwenye jeraha.

“Chatu Reticulated,ndiye nyoka mrefu zaidi duniani ambaye huua kwa kukaba katika mawindo yake,” amefafanua mtaalamu huyo.

Siku ya Nyoka Duniani, iliwekwa ili kuwasaidia watu kujifunza zaidi kuhusu nyoka na mchango wao mkubwa katika mazingira yetu.