Polisi waokota miili ya watu wanne, upo wa mwanamke

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 09:51 PM Jul 14 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi

Jeshi la Polisi mkoani Tanga, limesema limeokota miili ya watu wanne, ukiwamo wa binti mwenye umri wa miaka 24.

Taarifa iliyotolewa kwa umma leo Julai 14, 2025 na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Tanga, Almachius Mchunguzi imesema kuwa miili hiyo imeokotwa katika maeneo tofauti wilayani Handeni, mkoani humo.

Imesema miili miwili imebainika baada ya uchunguzi na kwamba mmojawapo ni wa Benard Wilson Masaka (43), aliyekuwa  mfanyabiashara wa nyama (Bucha) na mkazi wa Manispaa ya Morogoro.

Imesema mauaji ya mfanyabiashara huyo yanahusishwa na wivu wa kibiashara, na tayari watuhumiwa wamekamatwa na kufikishwa  mahakamani. 

Imetaja tukio lingine ni kuokotwa kwa mwili wa mwanamke mmoja katika Kijiji cha Mkata Wilaya ya Handeni, mnamo Februari 28 2025, ambapo uchunguzi ulibaini kuwa ni Fatuma Athuman (24), mkazi wa Kidereko, Handeni. 

"Watuhumiwa wanne wanaotuhumiwa kuhusika na mauaji ya mwanamke huyo wamekamatwa, na uchunguzi wa tukio hilo unaendelea kukamilishwa, ili hatua nyingine za kisheria ziweze kuchukuliwa.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Tanga linaendelea kushirikiana na Mikoa mingine kuhakikisha wahalifu wote wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria, na linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa taarifa kwa wakati kuhusu viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao," imefafanua.

Imeongeza kuwa: "Miili mingine miwili ya wanaume, ambayo bado haijatambuliwa, ilikutwa imetupwa porini katika maeneo tofauti ndani ya Wilaya ya Handeni, na inaendelea kuhifadhiwa kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi zaidi."