Rostam Aziz: Maudhui mengi yanayoongoza mijadala kuhusu Tanzania hayatoki ndani ya nchi

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 06:05 PM Jul 15 2025
Mfanyabiashara maarufu katika mataifa ya Afrika Mashariki, Rostam Aziz.
Picha:Mtandao
Mfanyabiashara maarufu katika mataifa ya Afrika Mashariki, Rostam Aziz.

Mfanyabiashara maarufu katika mataifa ya Afrika Mashariki, Rostam Aziz, amesema changamoto kubwa inayoikabili sekta ya habari nchini kwa sasa, ni maudhui mengi yanayoongoza mijadala kuhusu Tanzania hayatoki ndani ya nchi.

Amesema maudhui hayo, ni yale yanayozalishwa na kusambazwa na watu walioko nje ya mipaka yetu, watu wasioguswa na sheria zetu, mila zetu, wala misingi ya jamii yetu.

Rostam, mwanasiasa mkongwe na Mwenyekiti Taifa Group of Companies, akizingumza leo (Julai 15,2025) katika mkutano wa pili wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA) na Maadhimisho ya Miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania (MCT).

"Lakini changamoto yetu kubwa leo ni hii:
Maudhui mengi yanayoongoza mijadala kuhusu Tanzania hayatoki ndani ya nchi. Yanazalishwa na kusambazwa na watu walioko nje ya mipaka yetu, watu wasioguswa na sheria zetu, mila zetu, wala misingi ya jamii yetu.


...Watu hawa mara nyingi hawana hisa katika amani yetu, hawana uwekezaji katika maendeleo yetu, na hawawajibiki kwa madhara ya maneno yao.


Zaidi ameeleza, "Leo hii, chini ya uongozi thabiti wa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, uhuru katika sekta ya habari umeimarika, wajibu umezingatiwa na weledi unazidi kustawi."

AI imetawala mitandao ya kijamii

Kuhusu kukua kwa matumizi ya akili unde, Rostam Aziz, amesema hatalitendea haki jukwaa hilo kama ataongea walau kwa uchache, kuhusu zama mpya tunazoishi nazo, ambapo tasnia ya habari imetawaliwa zaidi na mitandao ya kijamii matumizi ya artificial intelligence yaani AI (akili unde).

"Ninazungumzia haya si tu kama mfanyabiashara, wala si tu kama raia, bali kama mtu anayeamini kuwa roho ya taifa inaweza kujengwa au kubomolewa na uadilifu wa mazingira ya habari katika jamii yetu.


"Tunaishi katika zama mpya — ambapo vita si tena kwenye uwanja wa mapambano wa kawaida, bali vinafanyika mtandaoni. Silaha siyo tena ni bunduki, bali algorithms. 


"Kila simu ya mkononi imekuwa kipaza sauti. Kila “like” au “share” kwenye majukwaa ya mitandao ya kijamii ni kura ya maoni. Na kila uongo usiopingwa, hatimaye huwa sehemu ya majadiliano ya taifa na hatimaye kuwa sehemu ya kumbukumbu ya taifa."