Dodoma kuzindua Mpango Mkakati wa Kukuza Utalii Agosti 4

By Ibrahim Joseph , Nipashe
Published at 05:03 PM Jul 15 2025
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.
Picha: Ibrahim Joseph
Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, amesema Mkoa huo unatarajia kuzindua mpango mkakati wa kukuza utalii kwa lengo la kuinua uchumi wa wananchi wake.

Akizungumza kuhusu mpango huo, Senyamule amesema uzinduzi unatarajiwa kufanyika Agosti 4, mwaka huu, ambapo mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabiti Kombo.

Amebainisha kuwa aina ya utalii unaolengwa katika mkakati huo ni ule wa utamaduni wa makabila makubwa yaliyopo katika Mkoa wa Dodoma ambayo ni Wagogo, Wasandawe, Warangi, na Waburunge. Alisema makabila hayo yana utajiri mkubwa wa mila na desturi ikiwemo ngoma, mapishi ya vyakula vya asili, na nyimbo za asili za kila kabila ambavyo vitakuwa kivutio kikubwa kwa watalii.

Aidha, Senyamule ametaja vivutio vingine vya utalii kuwa ni pamoja na hifadhi za misitu ya Swagaswaga na Mkungunero, ambazo zinapakana na Hifadhi ya Taifa ya Tarangire.

Ameongeza kuwa aina nyingine ya utalii inayopatikana katika Mkoa wa Dodoma ni utalii wa kilimo hususan kilimo cha zao la zabibu, ambalo linalimwa kwa wingi katika Mkoa huo na kuwa kivutio pekee nchini.

Mkuu huyo wa Mkoa amewataka wadau wa utalii wa ndani na nje ya nchi kushirikiana na Mkoa wa Dodoma katika kuutangaza utalii uliopo ndani ya Mkoa huo na Mikoa jirani.