KIINGEREZA kinaweza kuwa suala la maana kuliko ajenda za maendeleo? Kinaweza kutumiwa ‘kusanifu’.Hivi waweza kumshangaa mtu kisa anaongeza Kiingereza kitamu na cha kuvutia?
Kwa Rais wa Marekani Donald Trump, kuzungumza lugha hiyo kunaweza kuwa jambo la maana pengine kuliko ajenda za maendeleo ya Afrika.
Hilo linajiri wiki iliyopita Trump alipoguswa na kimombo cha Rais wa Liberia akimshangaza kuzungumza kwa ufasaha na kumtuliza Trump, anayesifika kwa kuwa na jazba muda wote.
Kiongozi wa Liberia, Joseph Boakai, anamchanganya Rais wa Marekani hadi kupoa moto na kuwa mpole kutokana na jinsi kiongozi huyo, alivyozungumza kwa ufasaha ung’eng’e, katika hadhira hiyo ambayo kilizungumzwa Kiingereza, Kifaransa na Kireno.
Rais wa Marekani akaonekana kushangazwa na ‘Kiingereza kikali’ japo ni lugha ya taifa ya Liberia, kisha akampongeza kweli kweli.
Lakini English ndiyo lugha rasmi ya Liberia ambayo ni taifa lililoanzishwa kwa idadi kubwa ya watumwa huru walioachiliwa kutoka Marekani, wakipewa nchi hiyo kuwa makazi.
Trump anamuuliza Joseph Boakai, ulijifunzia wapi kuongea kwa ufasaha hivyo?” Ulijifunzaje kuongea kwa uzuri hivyo?” Anaendelea, huku Boakai akichelewa kujibu. “Ulisoma wapi? Huko Liberia?”
Lakini akijua fika kuwa English ni lugha rasmi ya taifa hilo tangu miaka ya 1800, lakini Trump hakujali hilo, akaendeleza kejeli.
Mazungumzo hayo yakusifiwa yanajiri Ikulu ya White House, wakati wa mkutano kati ya Trump na viongozi watano wa Afrika Magharibi, unaozungumza mambo kadhaa kama misaada ya Marekani , biashara baina yao na sera za kigeni za Trump.
Siku hiyo mchana Rais Trump akipata chakula cha mchana na viongozi watano wa mataifa ya Afrika. Kulikuwa na lugha mbalimbali zikizungumzwa katika chumba hicho.
Vifaa vya sauti vilivaliwa ili tafsiri zisikike, kutoka kwa wakalimani. Liberia au ‘koloni’ la Marekani, imekuwa na uhusiano wa karibu na Washington kwa karne nyingi, kutokana na msukumo wa kuwahamisha watumwa walioachwa huru baada ya biashara ya watumwa kukomeshwa duninia.
NI DHARAU
Lakini nyumbani Liberia, kukawa na hisia tofauti, Foday Massaquio, mwenyekiti wa chama cha upinzani cha Congress for Democratic Change-Council of Patriots, anasema ingawa matamshi hayo yalikuwa mfano wa uhusiano wa Trump na viongozi wa kigeni, kile ambacho wengine wanaona kama sauti ya unyenyekevu na kusifia kilitawaliwa na ukweli kwamba viongozi hao ni Waafrika.
“Kwa kweli, inathibitisha kuwa nchi za Magharibi hazituchukulii kwa uzito zinaona ni Waafrika tu,” anasema. “Hili la Rais Trump lilikuwa dharau sana kwa marais wa Afrika.”
Msemaji wa Rais Boakai, Kula Fofana, analiambia shirika la habari la Associated Press la Ufransa kuwa:”Ninaamini waandishi wa habari, ni muhimu kuzingatia mijadala muhimu katika mkutano huo.”
“Tunaona ni jambo zuri kwamba Rais Trump anampongeza rais wetu kwa njia yake ya kuzungumza na kwa kuwa muwazi wakati wa mkutano,” anaongeza.
“Hata hivyo, tunatazamia kuona na kufikia masuala muhimu hasa kujihusisha na uhusiano wenye nguvu baina yetu na Marekani.”
SHANGWE NYUMBANI
Huko mitaani raia wa Liberia Alhamisi iliyopita wanasherehekea baada ya Rais Trump kumsifia kiongozi wao kwa kuzungumza Kiingereza kwa ufasaha. Akiongea katika kikao hicho cha biashara na uwekezaji kwenye Ikulu ya White House, kilichowashirikisha marais wa Guinea Bissau, Mauritania, Senegal na Gabon.
Mkutano huo ujadili jinsi mataifa hayo ya Afrika magharibi yangeimarisha uchumi wao na uwekezaji baina yao na Amerika. Baadhi ya raia wa Liberia katika jiji kuu la Monrovia wanasema ziara ya Ikulu na sifa za Trump kwa kiongozi wao zimeongezea nchi yao hadhi duniani.
“Jinsi rais wetu Boakai alivyozungumza kwa umakini ni wazi alikuwa na msingi imara wa elimu yake hapa Liberia. Hotuba yake ilifafanua jinsi anataka tunufaike kutokana na uhusiano wetu na Amerika,” anasema mwanahabari mmoja wa redio. Magazeti yote Liberia yalichapisha kauli za Trump kama habari kuu Ijumaa iliyopita.
“Boakai amewasilisha matakwa ya Liberia kwa ushujaa na umakini na amevutia wenyeji wake,” inasema taarifa kuu ya habari katika gazeti moja la nchi hiyo.
Habari kuu katika gazeti lingine zilisema ‘Liberia yapata alama zote katika mwaliko wa Trump’ huku taarifa hizo zikisisitiza Amerika si taifa dogo katika nyanja zote.
Akiongea katika kikao cha White House, Boakai alialika Amerika kusaidia nchi yake, inufaike na utajiri wa madini inayomiliki. Pia kupigia debe nchi yake kama yenye demokrasia Afrika akisema chaguzi zake huwa huru na mwamuzi ni raia.
Liberia ilianzishwa mwaka 1822 na Marekani kama kituo cha kuwapeleka watumwa walioachwa huru kutoka Amerika. Lilikua koloni na hatimaye ikawa mwanachama wa Jumuiya ya Madola, na kupata uhuru mnamo 1847.
Taifa hilo la Afrika ambalo mwanzo liliitwa koloni la Liberia, baadaye likaja kuwa ‘Commonwealth of Liberia’ au jumuiya ya madola ya Liberia (tafsiri isiyo rasmi) na hatimaye kujitangazia uhuru kama Jamhuri ya Liberia mnamo 1847 lugha yake ya taifa ni Kiingereza
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED