ACT Zanzibar: Wanachama 607 wachukua fomu kugombea nafasi mbalimbali

By Rahma Suleiman , Nipashe
Published at 05:03 PM Jul 15 2025
Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma Taifa wa chama hicho, Salum Bimani.
Picha: Mpigapicha Wetu
Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma Taifa wa chama hicho, Salum Bimani.

Wanachama 607 wa Chama cha ACT Wazalendo Zanzibar wamechukua fomu za kugombea nafasi mbalimbali za uongozi zikiwemo urais wa Zanzibar, ubunge, uwakilishi na udiwani kwa ajili ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Julai 15 katika Ofisi za chama hicho zilizopo Vuga, mjini Zanzibar, Katibu wa Habari, Uenezi na Mawasiliano kwa Umma Taifa wa chama hicho, Salum Bimani, amesema kati ya wagombea hao, wanawake 40 wamejitokeza kuwania nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani kwa majimbo 50 ya uchaguzi na wadi mbalimbali.

Ameeleza kuwa kati ya wanawake hao 40, wanawake 13 wameomba kugombea nafasi ya Uwakilishi, 15 Ubunge, na 12 Udiwani. Kwa upande wa viti maalum, amesema wanachama 52 wameomba kugombea Ubunge, 51 Uwakilishi, na 68 Udiwani.

Kuhusu nafasi ya Urais wa Zanzibar, Bimani amesema mgombea aliyejitokeza ni mmoja tu ambaye ni Othman Masoud Othman, Mwenyekiti wa chama hicho na pia Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar.

Ameongeza kuwa wagombea wote waliokuchukua fomu walifanikisha pia kuzirejesha, huku akifafanua kuwa gharama ya fomu ya Ubunge na Uwakilishi ilikuwa shilingi 100,000 na ya Udiwani shilingi 30,000.

Akizungumzia idadi ndogo ya wanawake waliojitokeza kugombea, Bimani amesema hali hiyo inachangiwa na vitisho pamoja na chaguzi zisizo na uadilifu, jambo linalowatisha wanawake wengi kuingia kwenye siasa. Amesema ni muhimu kuweka mazingira salama na huru ili kufikia usawa wa kijinsia wa asilimia 50 kwa 50 katika vyombo vya maamuzi.

Amehitimisha kwa kusema kuwa chama hicho kimeshakamilisha taratibu za awali za kura za maoni na hatua inayofuata ni vikao vya chama ili kuwapitisha wagombea wa mwisho kwa kila nafasi watakaowakilisha ACT Wazalendo katika Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.