Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), imewahoji watia nia 11 wa nafasi ya Ubunge katika Mkoa wa Kilimanjaro, kutokana na malalamiko ya rushwa yaliyowasilishwa.
Mkuu wa TAKUKURU mkoani humo, Mussa Chaulo, amesema malalamiko hayo kwa sasa wanaendelea kuyafanyia kazi, kwa kuyachakata, ili kuona ukweli wa malalamiko hayo ukoje.
Chaulo, alikuwa akizungumza jana (Julai 15, 2025) kwenye semina maalum ya mapambano dhidi ya rushwa katika Mji wa Moshi. Semina hiyo iliwahusisha watia nia wa uchaguzi mkuu 2025 wa nafasi ya Ubunge.
“Kabla ya uteuzi kuja, tayari tutakuwa tumeshapeleka taarifa. Kwa hiyo kabla ya kufanyika uteuzi, tayari kila taarifa tutakuwa tumepeleka, wale ambao tumekusanya mambo yao waliyoyafanya.
“Tumepokea malalamiko kadhaa katika ofisi yetu. Hatua ya kuchukua malalamiko, unayafanyia kazi, unachakata ili ujue kwamba kuna ukweli kwenye malalamiko hayo au hakuna malalamiko au ukweli ndani yake.
…Malalamiko ambayo sasa hivi tumefanyia kazi, ni malalamiko 11, ambayo tumeendelea kuyafanyia kazi na tunaendelea kuyachakata ili tuone ukweli wa malalamiko hayo yakoje.
"Kwa hiyo kipindi hiki cha uchaguzi kuna malalamiko mengine watu wanatengenezeana tuhuma ambazo sio sahihi na kwa hiyo TAKUKURU tunakuwa makini kuhakikisha kwamba kila tuhuma ambayo tunaipata tunaifanyia kazi kwa undani zaidi ili tuweze kupata uthibitisho kabla ya kufikia hatua nyingine. 11 wote tumewahoji tayari.”
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED