UONGOZI wa Klabu ya Singida Black Stars, umeuchagua Uwanja wa Benjamin Mkapa na Azam Complex vyote vya Dar es Salaam kama viwanja vyake vya nyumbani kwenye mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Singida Black Stars pamoja na Azam FC, zitaiwakilisha nchini kwenye michuano hiyo msimu ujao huku Simba na Yanga zikipeperusha bendera ya Tanzania kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Taarifa zilizopatikana jana jijini Dar es Salaam na kuthibitishwa na uongozi wa klabu hiyo, zimeeleza kuwa viwanja hivyo vimekidhi vigezo vya Shirikisho la Soka Afrika, CAF.
Tayari kupitia Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Singida Big Stars imewasilisha barua CAF ya kutumia viwanja hivyo viwili.
"Ni kweli, tutatumia viwanja hivyo kwenye mashindano yetu ya kimataifa..., ni viwanja ambavyo vimekidhi vigezo vya CAF, tunawataarifu mashabiki wetu hivyo ndio viwanja tutakavyotumia kwenye mashindano hayo ya kimataifa," alisema Hussein Masanza, Afisa Habari wa klabu hiyo.
Alisema Singida Black Stars inajipanga kuhakikisha inafanya vizuri kwenye mashindano hayo watakayoshiriki kwa mara ya kwanza msimu ujao.
Singida Black Stars imekata tiketi ya kushiriki mashindano hayo baada ya kufanikiwa kumaliza nafasi ya nne kwenye Ligi Kuu msimu uliopita ambapo itaungana na Azam FC waliomaliza nafasi ya tatu nyuma ya Simba na Yanga.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED