MSANII wa Bongo Fleva Omari Ally (Marioo) pamoja na msanii wa muziki wa singeli Dogo Patten wanatarajiwa kutumbuiza Julai 26 mwaka huu katika mchezo wa fainali utakaikutanisha timu ya vijana ya Yanga dhidi ya Safari Lager, mchezo ambao utachezwa kwenye uwanja wa KMC Mwenge.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Meneja wa Safari Lager Pamela kikui amesema maandalizi kuelekea kwenye mchezo huo yamekamilika huku akitoa wito kwa Watanzania kujitokeze kwa wingi.
“Ili kunogesha fainali hiyo tutakuwa na burudani ya mziki kutoka kwa Marioo pamoja Dogo Patten tunaomba watanzania waje kwa wingi kushuhudia vipaji vinavyotolewa na vijana,” amesema Kikui.
Meneja Habari wa Klabu ya Yanga Ally Kamwe amesema kabla ya mchezo huo kutakuwa na mchezo wa ufunguzi kati ya mashabiki wa timu hiyo dhidi ya wasanii mbalimbali wakiwemo wa muziki vichekesho pamoja na waigizaji.
“Mchezo huo utatanguliwa na mchezo wa ufunguzi utakaowakutanisha mashabiki wa Yanga na wasanii mbalimbali tunaomba watanzania wasiache kufika siku hiyo,” amesema Kamwe.
Amesema tiketi kwa ajili ya mchezo huo tayari zimeanza kuuzwa na kuwataka watanzania kuchangamkia fursa hiyo ili kuepusha usumbufu siku ya mchezo.
Naye, Mkurugenzi wa mashindano wa klabu hiyo Ibrahim Mohamed ameitaka timu ya Safari Lager kufwata maelekezo wanayopewa na wachezaji wa zamani pindi wanapokuwa mazoezini ili waweze kutimiza ndoto zao.
“Kwa upande wetu tupo kwa ajili ya kuinua vipaji vya vijana tukiridhishwa na viwango vyenu hatutawaacha tutawachukua na kuwaendeleza,” amesema Mohamed.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED