Pamba FC kuboreshwa upya - RC Mtanda

By Augusta Njoji , Nipashe
Published at 05:08 PM Jul 16 2025
news
Picha Mtandao
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda

Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema maandalizi makubwa yanaendelea kuhakikisha timu ya Pamba SC inakuwa imara zaidi kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara.

Ametoa maelekezo ya kutafuta benchi jipya la ufundi pamoja na kufanya usajili wa wachezaji bora watakaoweza kupigania hadhi ya timu hiyo na kufanikisha matokeo mazuri msimu ujao.

Akizungumza jijini Dodoma wakati wa kutoa taarifa kuhusu mafanikio ya serikali katika kipindi cha miaka minne, Mtanda amesema mpango waliouweka ili kuhakikisha Pamba SC inabaki kwenye ligi kuu umetimia kwa asilimia 100.

“Kwa zaidi ya miaka 23 Pamba ilikuwa haishiriki ligi kuu na ilicheza ligi ya daraja la kwanza. Ilikuwa muhimu kuweka mikakati ya muda mrefu kuhakikisha timu inarejea na kusalia ligi kuu. Tunajivunia kuona malengo yetu yamefikiwa,” amesema Mtanda.

Aidha, ametoa wito kwa viongozi wa timu hiyo kuhakikisha fedha zinazotolewa na halmashauri kwa ajili ya maendeleo ya timu zinatumika ipasavyo, kwa mujibu wa malengo yaliyopangwa.

1
Amesisitiza kwamba serikali ya koa bado ina vipaumbele vingine muhimu vya maendeleo vinavyohitaji rasilimali.

“Tumejipanga kuifanya Pamba SC iwe timu ya ushindani mkubwa na kuendelea kubaki ligi kuu, sambamba na hadhi ya Mkoa wa Mwanza. Hivyo, nawasihi viongozi wa timu kuhakikisha fedha zilizotolewa zinatumika kikamilifu kwa malengo yaliyokusudiwa, kwani Serikali ina miradi mingi ya maendeleo inayohitaji utekelezaji,” ameongeza.

Pamba SC ilirejea kwenye Ligi Kuu msimu wa 2024/225 baada ya kukaa nje ya ligi hiyo kwa zaidi ya miongo miwili. Sasa, timu hiyo imeweka mkakati wa kufanya maboresho makubwa ndani ya kikosi chake ili kuhakikisha inaendelea kushindana na kusalia kwenye ligi kuu kwa msimu ujao.