Polisi: Hatuhusiki kutoweka kijana Kongowe

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 11:18 AM Jul 17 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi Salim Morcase.
Picha: Mpigapicha Wetu
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi Salim Morcase.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Pwani limekanusha vikali taarifa zinazoeleza kuwa Mkuu wa Kituo Kidogo cha Polisi Kongowe, Wilaya ya Kibaha, alihusika katika kumkamata kijana Hussein Abdallah Mkama mnamo Mei 19, 2025.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Kamishna Msaidizi wa Polisi Salim Morcase, amesema taarifa hizo hazina ukweli wowote. Kamanda Morcase alieleza kuwa Hussein anadaiwa kukamatwa na watu wasiofahamika akiwa eneo la Ungindoni, Kongowe, kisha kuchukuliwa na kupelekwa kusikojulikana.

Kwa mujibu wa Kamanda huyo, malalamiko kuhusu tukio hilo yaliwasilishwa na baba wa kijana huyo, Abdallah Mkwama, ambaye alilitaja Jeshi la Polisi kupitia kwa Mkuu wa Kituo cha Kongowe kwamba alikuwepo eneo la tukio wakati wa ugomvi baina ya mwanawe na rafiki yake anayetambulika kwa jina maarufu la Zarumenda.

Hata hivyo, Kamanda Morcase ameeleza kuwa uchunguzi wa awali umebaini kuwa siku ya tukio la Mei 19, Mkuu wa Kituo cha Polisi Kongowe alikuwa na ruhusa maalumu ya kikazi iliyotolewa na Mkuu wake wa Himaya, kwa ajili ya kwenda kushiriki mazishi ya askari mwenzao huko Msangani Kwamatiasi, Kibaha – mazishi ya aliyekuwa askari wa Morogoro, marehemu Mwikwabe.

Aidha, Kamanda ameongeza kuwa kwa utaratibu rasmi wa kazi, Kituo Kidogo cha Polisi Kongowe hufungwa saa 12 jioni, ilhali tukio hilo linadaiwa kutokea majira ya saa moja usiku.

TUKIO LILIVYOTOKEA

Akieleza kuhusu tukio lenyewe, Kamanda Morcase amesema Jeshi la Polisi lilipokea taarifa za kupotea kwa kijana Hussein mnamo Mei 21, 2025, kutoka kwa baba yake mzazi, na mara moja walifungua jalada la uchunguzi namba KBA/CID/PE/31/2025.

Katika hatua za awali za uchunguzi, Polisi waliwahoji mashahidi mbalimbali akiwemo Asia Mbonde (shemeji wa Hussein) na Fatuma Omari.

Kwa mujibu wa maelezo ya Asia Mbonde, siku ya tukio aliokuwa ameketi na Hussein dukani majira ya saa moja usiku, alifika kijana anayetambulika kama Zarumenda ambaye ni rafiki wa karibu wa Hussein. Zarumenda alimuita Hussein na kwenda naye umbali wa takribani mita 30 kwenye kichochoro chenye giza ambapo walionekana kugombana.

Asia alieleza kuwa muda mfupi baadaye, walitokea watu wanne waliodhaniwa kuwa ni mgambo wa eneo hilo, ambao waliondoka na Hussein kuelekea kusikojulikana.

Kwa upande wake, Fatuma Omari ameeleza kuwa alimwona Hussein akiwa amelala chini huku akishambuliwa na vijana wanne ambao hakufanikiwa kuwatambua kutokana na giza kutawala eneo hilo.

HATUA ZAIDI ZA UCHUNGUZI 

Kamanda Morcase amesisitiza kuwa Jeshi la Polisi linaendelea na uchunguzi wa kina juu ya tukio hilo, na juhudi za kumtafuta kijana Hussein pamoja na Zarumenda zinaendelea kwa nguvu zote.

Aidha, amewataka wananchi kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi kwa kutoa taarifa yoyote itakayosaidia kupatikana kwa kijana huyo au kuwafichua wahusika wa tukio hilo.

“Tunalichukulia tukio hili kwa uzito mkubwa. Hatuwezi kuruhusu mtu yeyote kupotea bila kuchukua hatua. Tunawatoa hofu wananchi kwamba upelelezi huu utaendelea kwa weledi na uwazi,” amehitimisha Kamanda Morcase.