IMEELEZWA kuwa mradi wa ujenzi wa bomba la Mafuta ghafi la Afrika Mashariki (EACOP), hauna athari za kimazingira kutokana na serikali kuweka sera nzuri na teknolojia rafiki kwa mazingira, ili kulinda bayoanuai wakati wa upitishaji wa bomba la mradi chini ya Mto Zigi
Mhandisi Thomas Mhando, ambaye ni msimamizi wa mradi wa ujenzi wa bomba kuvuka Mto Sigi, kinachojumuisha ulazaji wa bomba na uchorongaji kwa ajili ya kuvusha bomba chini ya mto , ameelezea maendeleo ya mradi kwenye eneo hilo, sambamba na kuhakikisha mazingira yanalindwa kipindi chote cha kusimika bomba hilo
Ameongeza kuwa, wakati wa utekelezaji wa mradi kupeleka maji EACOP, walikubaliana kuwawezesha pia wananchi wa vijiji saba vilivyoko karibu na maeneo ya utekelezaji wa mradi kwa kuhakikisha wanapatiwa maji chini ya mradi wa makubaliano, jumla ya Sh. bil 2.728 zilitolewa na EACOP kutekeleza mradi wa maji ili wananchi pia wapate maji.
Awali akizungumza kwenye eneo la utekelezaji wa mradi huo, Mratibu wa kitaifa wa Mradi kutoka TPDC, Asiadi Mrutu, amesema kwa sasa uvushaji wa bomba kwenye Mto Sigi unaendelea vizuri na umefikia asilimia 63 na unatarajiwa kukamilika Novemba 2025 na ameishukuru NEMC kwa kusimamia suala la mazingira kwenye mradi huo kwa kuhakikisha wanatembelea mara kwa mara, ili kuona kazi inavyoendelea.
Ameishukuru serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, kwa ujio wa mradi kutoka Hoima nchini Uganda hadi Chongoleani mkoa wa Tanga na kueleza kuwa umeleta mabadiliko ya kiuchumi kwa mkoa wa Tanga.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED