SEKTA binafsi wameiomba serikali kuwekeza kwenye rasilimali watu nchini hususani vijana, ili nchi kupiga hatua katika maendeleo.
Rostam Azizi ambaye ni mwakilishi wa sekta binafsi amesema hay oleo, Julai 17, 2025 katika uzinduzi wa Dira ya Taifa 2050, uliofanyika jijini Dodoma.
Amesema ili kufanikisha hilo kuanzishwe mfuko wa vijana ambao utakiwa na bajeti maalum ambayo itasomesha vijana ndani na nje ya nchi kwenye fani za Akili Unde (AI), sayansi na takwimu pamoja na fani nyingine.
Amefafanua zaidi kuwa huo utakuwa ni uwekezaji wa kimkakati, huku akishauri kuimarishwa kwa vyuo vya ndani kuhakikisha vinatoa wataalam wenye vigezo vya kimataifa katika fani zilizoanishwa.
"Ni muhimu kuendeleza viongozi kwa kuwapa fursa za kushiriki mafunzo mbalimbali ya uongozi ndani na nje ya nchi lakini pia Balozi ziwe na jukumu la kurudisha wataalam wanaosoma kozi hizo nchini," amesema Aziz.
Aidha amesema serikali inapaswa kuweka mkakati maalum wa kulinda na kujenga sekta binafsi ya ndani, kwa kuwa ndio watakaoijenga nchi yao.
Mbali na hilo Rostam, ameipongeza serikali kwa kupokea maoni ya sekta binafsi, amesema moja ya maoni waliyotoa ni kuhakikisha ifikapo 2050, uchumi wa taifa uwe umefikia Sh. trilioni moja.
Amesisitiza kuwa hakuna nchi inayojengwa na wageni, bali wazawa, hivyo inanapaswa kuwa watekelezaji wa ahadi au mipango inayopangwa.
"Sisi watanzania ni wazuri wa kupanga mipango lakini kwenye utekelezaji tunasuasua," amesema Rostam.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED