Wakili Shabaan Marijani amesema watu wote waliyotajwa katika zuio la Mahakama la kutokushiriki shughuli zozote za kisiasa katika Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hawaruhusiwi hata kuzungumza na vyombo vya habari.
Aidha, amesema wakitaka kuzungumza na vyombo hivyo wasizungumze masuala ya chama, waeleze mambo mengine ambayo hayaingiliani na amri ya zuio hilo lililotolewa Juni 10,2025 na Jaji Hamidu Mwanga.
Wakili Marijani amesema hayo leo jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na upotoshaji uliyokuwa ukiendelea kuhusiana na zuio lililotokana na shauri dogo namba 8960/2025 katika Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam.
"Hawatakiwi hata kuzungumza na waandishi wa habari kwa sababu tayari Mahakama ilishatoa amri ya zuio hapo wanakuwa wamekiuka amri hiyo," Amesema Wakili Marijani
Kwa upande wake, Wakili Gizo Simfukwe amesema Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imetoa ufafanuzi wa wahusika 10 wa zuio hilo kutokana na baadhi ya watu kujiondoa kwamba hawahusiki.
"Kutokanana na upotoshaji huu na sisi kama wanasheria tunawawakilisha wateja wetu waliyofungua hii kesi tulimuandikia Msajili wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo ya Dar es Salaam barua kuomba ufafanuzi wa kisheria kwamba Je! lile zuio lililotolewa linawahusu wakina nani," Amesema Wakili Simfukwe
Amesema kuwa wamepokea barua ya majibu kutoka kwa Msajili ya Julai 14,225 ambayo hata wenzao wa upande wa pili wa kesi hiyo na wao wamepewa nakala yake, ambapo baadhi ya watu walisema zuio ni la Bodi ya Wadhamini na Katibu Mkuu.
"Huu ndiyo ufafanuzi wa kisheria wa Msajili ameandika na kutoa ufafanuzi huu kwamba hawa wote waliyotajwa hapa wamezuiliwa hadi pale kesi ya msingi itakaposikilizwa na kutolewa uamuzi,".
Amesema Wakili Simfukwe
Aliwataja watu hao, kuwa ni Bodi ya Wadhamini Chadema, Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Kaimu Mwenyekiti wa Chadema Taifa, Makamu Mwenyekiti Chadema Tanzania Bara au Kaimu Makamu Mwenyekiti Chadema Tanzania Bara.
Wengine ni Makamu Mwenyekiti Chadema Tanzania Zanzibar au Kaimu Makamu Mwenyekiti Chadema Tanzania, Zanzibar, Katibu Mkuu Chadema au Kaimu Katibu Mkuu Chadema, Naibu Katibu Mkuu Chadema Tanzania bara au Kaimu Naibu Katibu Mkuu Chadema Tanzania Bara, Naibu Katibu Mkuu Chadema Tanzania Zanzibar au Kaimu Naibu Katibu Mkuu Chadema Tanzania Zanzibar.
Pamoja na viongozi wote na katika ngazi zote iwe ni viongozi walioteuliwa moja kwa moja katika nafasi zao za kiuongozi au wanaokaimu katika nafasi zao za uongozi na mfanyakazi au wakala au mtu yeyote yule anaefanya kazi hizo kwa niaba ya Chadema.
"Au aliyepewa maelekezo au kuiwakilisha Chadema, atakayefanya kazi zozote za kisiasa kwa kutokea Taifa, Mkoa, Wilaya, Halmashauri, Tarafa na maeneo yote nchini kwa pande zote mbili za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania bara na Tanzania Zanzibar,"alisema Wakili Simfukwe
Wakili Simfukwe alisema madhara ya mtu atakayekwenda kinyume na uamuzi wa Mahakama atakuwa anatenda kosa la jinai ambalo linajulikana na kudharau amri ya Mahakama na pia anaweza kuchukuliwa hatua zingine za kimadai kwa mujibu wa sheria.
"Kwa sababu Mahakama inapoelekeza na wewe ukaenda kinyume na Mahakama kwa kujificha kwenye mwavuli kwamba mimi hainuhusu huo utakuwa ninuvunjaji wa sheria. Tumeamua kutoa ufafanuzi huu kwa umma kuondoa upotoshaji kwa baadhi ya watu," Amesema
Watu hao waliyozuiliwa kutokana na kesi ya madai namba 8960/2025 iliyofunguliwa na aliyewahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Chadema Zanzibar, Said Issa Mohamed, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Mahakama ilikubali maombi hayo na zuio lililotolewa kwa mujibu wa amri (order) ya Jaji Hamidu Mwanga katika shauri dogo la madai namba 8960 la mwaka 2025, wakati uamuzi wa maombi katika kesi kuu ya madai namba 8323/2025, Mahakama ilitoa zuio hilo.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED