Uhusiano Somalia, Tanzania waimarika

By Gwamaka Alipipi , Nipashe
Published at 01:08 PM Jul 17 2025
Balozi Ilyas Ali Hassan
Picha: Mpigapicha Wetu
Balozi Ilyas Ali Hassan

Nchi ya Somalia imeingia makubaliano tisa na Tanzania katika kipindi cha miezi saba, pamoja na kupanua wigo wa kidipolomasia katika nchi za Malawi, Comoro.

Mkakati huu wa kimataifa umetokana na juhudi kubwa za sera za kimataifa za Somalia katika ukanda wa Afrika Mashariki tangu mwanzoni mwa miaka ya 1990 na unasimamiwa na Balozi Ilyas Ali Hassan, mwakilishi wa Somalia nchini Tanzania na mwakilishi wa kudumu katika Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Makubaliano hayo yalianza Desemba 19 mwaka jana jijini Mogadishu wakati ujumbe wa mawaziri kutoka Tanzania ulioongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje, Mahmoud Thabit Kombo kusaini makubaliano matano na wenzao wa Somalia.

Makubaliano hayo yalihusisha ushirikiano wa mambo ya nje, magonjwa, utalii, mafunzo ya ulinzi na ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Somalia.

Taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje ya Somalia ilitaja makubaliano hayo kama msingi wa ushirikiano endelevu wa kikanda.

Januari 29 mwaka huu, Dar es Salaam iliandaa ziara nyingine ambapo Waziri wa Mambo ya Nje, Ahmed Moallim Fiqi alisaini makubaliano ya ulinzi na usalama, mkataba unaowezesha raia wa Somalia waliokamatwa Tanzania kutumikia vifungo vyao nchini mwao.

Pia makubaliano ya Lugha ya Kiswahili yenye lengo la kurahisisha njia ya Somalia kujiunga na Jumuiya ya Afrika Mashariki.

Ushirikiano huu ulitangazwa Julai 1 mwaka huu wakati Somalia ilipoadhimisha miaka 65 ya Uhuru wake katika ubalozi wa nchi hiyo uliopo Kurasini, uliofunguliwa upya na Serikali hizo mbili zikasaini upya mkataba wa usafiri wa anga.

Makubaliano haya yatairuhusu Air Tanzania kuanzisha safari za moja kwa moja kutoka Dar es Salaam hadi Mogadishu katika wiki chache zijazo na kuahidi ufikiaji wa mashirika ya ndege ya Somalia mara tu vigezo vya usalama vitakapofikiwa.

Balozi Ilyas alisema usafiri wa anga ni alama ya mabadiliko.

"Wakati mjasiriamali wa Somalia anapopanda ndege asubuhi kwenda Dar es Salaam na kutua kabla ya chakula cha mchana, mipaka haiwi tena vizuizi bali inakuwa viunganishi," alisema

Wakati Tanzania ikibaki kuwa nguzo kuu ya juhudi za Somalia, jukumu la balozi sasa linapanua wigo wa ushirikiano.

Julai 3 mwaka huu Balozi Ilyas alikabidhi hati zake za utambulisho kwa Rais Lazarus Chakwera katika Ikulu ya Kamuzu jijini Lilongwe, akiahidi ushirikiano katika biashara, kilimo na usalama.

Siku sita baadaye, alifanya vivyo hivyo jijini Moroni, ambapo Rais wa Comoro, Azali Assoumani alikaribisha nia ya Somalia ya kuimarisha uhusiano wa baharini na maendeleo.

Wafanyabiashara jijini Dar es Salaam tayari wameiona fursa. Wakala wa mizigo wanasema kuwa safari ya saa tatu kwenda Mogadishu inaweza kupunguza gharama za mizigo kwa theluthi moja kwenye njia kuu kama samaki kuelekea kaskazini na bidhaa za viwandani kuelekea kusini.

Maofisa wa bandari wanasema kuwa usafiri wa anga mara nyingi huvutia kiasi kikubwa cha mizigo ya baharini kadri wafanyabiashara wanavyotumia fursa ya ushirikiano kati ya anga na bahari. Wataalamu wa elimu nao wanaeleza hivyo hivyo dhamira hiyohiyo.

Kwa mujibu wa makubaliano ya ufadhili wa masomo ya Mogadishu, wanafunzi wa uhandisi na sayansi ya afya kutoka Somalia watajiandikisha katika vyuo vikuu vya Tanzania kuanzia Januari 2026.

Ilyas anasema: "Uaminifu wetu unategemea kubadilisha saini kuwa huduma. Ikiwa, mwakani, wasafiri watakuwa wanakata tiketi za ndege za moja kwa moja, wanafunzi watazungumza Kiswahili kwa ujasiri na doria zetu za pamoja zitakuwa zinalinda maeneo yale yale, basi tutajua kuwa makubaliano haya yamefanikiwa."  anasema Ilyas