Upasuaji ubongo wafikia wagonjwa 4,000 Mloganzila

By Christina Mwakangale , Nipashe
Published at 05:26 PM Jul 17 2025
Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Mgongo wa Mishipa ya Fahamu, kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk. Raymond Makundi
Picha: Mnh-Mloganzila
Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Mgongo wa Mishipa ya Fahamu, kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk. Raymond Makundi

IDADI ya wagonjwa wa nje (OPD) wanaofanyiwa upasuaji wa ubongo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, imeongezeka kutoka 2,000 kwa mwaka hadi kufikia 4,000 kwa kipindi cha miaka saba iliyopita.

Pia, imebainisha kwamba wagonjwa wa ndani wanaofanyiwa upasuaji kwa kipindi hicho, imeongezeka kutoka 100 hadi 400 kwa mwaka.

Bingwa Mbobezi wa Upasuaji Mgongo wa Mishipa ya Fahamu, kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)-Mloganzila, Dk. Raymond Makundi, alisema hayo Dar es Salaam, akizungumzia kuhusu huduma hiyo.

Dk. Makundi ambaye pia ni Kaimu Mkuu wa Idara ya Upasuaji Ubongo hospitali hiyo, amesema uwekezaji mkubwa wa vifaatiba umeongeza ubora wa huduma ikiwamo vyumba vya kisasa.

Amesema idara hiyo ambayo ilianza miaka saba iliyopita, tayari imehudumia wagonjwa tofauti watu wazima na watoto, huku wigo wa aina za upasuajia ukiongezeka.

“Mwanzoni tulikuwa tunahudumia watoto wenye mgongo wazi na vichwa vikubwa, lakini sasa pamoja na wenye uvimbe kichwani, wagonjwa wa ajali na waliopata maambukizi.

“Mafanikio haya yanatokana na uwekezaji mkubwa, hospitali hii ni ya kisasa, pia ina mchanganyiko wa mabingwa bobezi,” amesema Dk. Makundi.