Miss World,Afrika na Doris Mollel Foundation watembelea watoto njiti Mwananyamala

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 03:10 PM Jul 17 2025
Miss World,Afrika na Doris Mollel Foundation watembelea watoto njiti Hospitali ya Mwananyamala
Picha:Mpigapicha Wetu
Miss World,Afrika na Doris Mollel Foundation watembelea watoto njiti Hospitali ya Mwananyamala

Mrembo wa Dunia (Miss World) (@suchaaata), pamoja na Mrembo wa Afrika (@hasset_dereje) pamoja na mdau wa masuala ya afya na mitindo Mustafa Hassanali (@mustafahassanali), wametembelea wodi ya watoto njiti katika Hospitali ya Mwananyamala kwa kushirikiana na Doris Mollel Foundation.

Katika ziara hiyo ya kugusa maisha, iliyofanyika jana Julai 16,2025 warembo hao wameonyesha kuguswa na hali ya watoto njiti na kazi kubwa inayofanywa na madaktari, wauguzi pamoja na taasisi ya Doris Mollel Foundation katika kutoa huduma bora kwa watoto hao wenye uhitaji mkubwa wa uangalizi maalum.

Akizungumza baada ya ziara hiyo, Miss World, @suchaaata alieleza kufurahishwa na juhudi na moyo wa kujitolea unaoonyeshwa na watumishi wa afya, huku akiweka bayana dhamira yao ya kusaidia juhudi hizo kwa kuchangia vifaa tiba vinavyohitajika kwa ajili ya kuokoa maisha ya watoto njiti.

Kwa upande wake Miss Africa, @hasset_dereje aliwahakikishia watanzania kuwa ujumbe walioupokea utawawezesha kuendeleza kampeni za kimataifa kwa ajili ya kusaidia hospitali nyingine nchini hususan maeneo ya pembezoni ambako huduma kama hizo bado hazijafika kwa ukamilifu.

Naye Mustafa Hassanali alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya mashirika ya kijamii, serikali na wadau wa kimataifa katika kuhakikisha watoto wote wanaozaliwa kabla ya wakati wanapata haki ya kuishi na huduma stahiki.

Kwa pamoja walipongeza jitihada za Doris Mollel Foundation kwa mchango wake mkubwa katika kuboresha huduma za afya kwa watoto wachanga nchini Tanzania na kuahidi kuendelea kuwa mabalozi wa kampeni hiyo kwa ngazi ya kikanda na kimataifa.