Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Ali Mwinyi, amewakabidhi tuzo maalumu za shukrani kwa wenyeviti na wakurugenzi wa Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), wakiwemo waliowahi kuitumikia tume hiyo na waliopo sasa.
Miongoni mwa waliotunukiwa ni aliyekuwa Mwenyekiti wa ZEC, marehemu Jecha Salim Jecha, aliyejizolea umaarufu mkubwa katika uchaguzi wa mwaka 2015.
Tuzo hizo zilitolewa leo Julai 16, sambamba na ufunguzi wa jengo jipya la Tume ya Uchaguzi Zanzibar, lililopo Maisara.
Akihutubia katika hafla hiyo, Rais Dk Mwinyi amesisitiza kuwa uchaguzi mkuu haupaswi kuwa chanzo cha mifarakano au kuvuruga amani ya nchi, akieleza kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo.
Ametoa wito kwa wananchi wote kuwa walinzi wa amani kabla, wakati na baada ya uchaguzi, huku akisisitiza wajibu wa serikali kuwatumikia wananchi kwa misingi ya haki na usawa bila kujali itikadi zao.
Dk Mwinyi ameeleza kuridhishwa kwake na namna uandikishaji wa wapiga kura wapya ulivyofanyika kwa utulivu, akisema changamoto ndogo zilizojitokeza zilituliwa kwa wakati.
Aidha, ameongeza kuwa kiwango cha uwazi katika maandalizi ya uchaguzi kinatoa matumaini kuwa uchaguzi ujao utakuwa huru na wa haki.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED