Maharagwe ya TARI Bean 6 kupunguza utapiamlo kwa watoto, wajawazito

By Jaliwason Jasson , Nipashe
Published at 10:06 PM Jul 16 2025
Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Selian, Dk. Caresma Chuwa
Picha Mpigapicha Wetu
Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Selian, Dk. Caresma Chuwa

Kituo cha Utafiti wa Kilimo cha TARI Selian, Arusha, kimetangaza kuwa maharagwe ya aina ya TARI Bean 6, yaliyofanyiwa utafiti wa kina, yanaweza kusaidia kukomesha utapiamlo kwa watoto wachanga, wajawazito, na vijana rika balehe nchini.

Hii ni kwa sababu ya uwingi wa madini muhimu kama chuma na zinki yaliyomo ndani yake.  

Kauli hiyo ilitolewa leo na Mkurugenzi wa Kituo cha TARI Selian, Dk. Caresma Chuwa, alipokuwa akitoa mafunzo kwa wakulima wa Kata ya Kiru, Kijiji cha Kiru Six, wilayani Babati, mkoani Manyara, wakati wa sherehe za **Siku ya Mkulima Shambani.  

Dk. Chuwa amesema kuwa ukosefu wa madini kama chuma na zinki kwa watoto, wajawazito, na vijana umeendelea kuwa changamoto, lakini matumizi ya maharagwe ya TARI Bean 6 yanaweza kuwa tiba kwa tatizo hilo.  

"Haya maharagwe ya TARI Bean 6 yana wingi wa chuma na zinki, na ndiyo suluhisho la kupunguza utapiamlo hasa kwa watoto na wanawake wajawazito nchini," amesema Dk. Chuwa.  

Sabina Bululu, mkazi wa Kijiji cha Kiru Six, ameshukuru TARI Selian kwa kuwapa elimu hiyo na kuwaomba wapate huduma ya kupimwa udongo ili waweze kuzalisha kwa tija zaidi.  

Kwa upande wake, Ofisa Kilimo wa Halmashauri ya Wilaya ya Babati, Paschal Mahetu, amezishukuru taasisi za utafiti kwa kusambaza maarifa na kuahidi kuwasaidia wakulima kwa kupima udongo bure ili kuboresha uzalishaji.  

"Tunawaomba TARI Selian kuendelea kufikia vijiji vingine kwa mafunzo kama haya kwa manufaa ya wakulima," amesema Mahetu.