Mambo matatu yaibeba Tanzania malipo ya kidijitali

By Restuta James , Nipashe
Published at 06:20 PM Jul 16 2025
Mambo matatu yaibeba Tanzania malipo ya kidijitali
Picha: Mpigapicha Wetu
Mambo matatu yaibeba Tanzania malipo ya kidijitali

Ongezeko la matumizi ya simu na mtandao, kukua kwa kasi kwa sekta ya wajasiriamali wadogo na wa kati, pamoja na jitihada za ujumuishaji wa kifedha, kumetajwa kuibeba Tanzania malipo kidijitali.

Akizungumza Dar es Salaam leo Julai 16, 2025, kwenye maadhimisho ya siku ya Visa Tanzania, Mkuu wa kampuni ya malipo ya kidijitali ya Visa kwa Ukanda wa Kusini na Mashariki mwa Afrika, Michael Berner, amesema jitihada za Tanzania zinatoa fursa ya kuunda mfumo wa malipo wenye ubunifu na unaojumuisha watu wote.

Amesema maeneo hayo matatu yameifanya kampuni hiyo kufungua ofisi zake nchini, kama hatua muhimu za kuimarisha ushiriki wake katika kukuza matumizi ya malipo ya kisasa nchini Tanzania na nchi jirani.

Berner aliyasema hayo wakati ambao Tanzania imeadhimisha kwa mara ya kwanza siku Visa, iliyoongozwa na kaulimbiu ya ‘Kujenga Mustakabali wa Malipo Nchini Tanzania’, ambayo imewakutanisha wadau kutoka sekta ya fedha na teknolojia ya kifedha.

Amesema matokeo ya utafiti wake wa hivi karibuni, yanaonesha kwamba matumizi ya njia za kidijitali yanafaida za kiuchumi na kijamii, zikiwemo kupunguza matumizi ya fedha taslimu, kuongeza uwazi wa kifedha, na kuimarisha ujumuishaji wa makundi yasiyofikiwa kirahisi na huduma za kifedha.

Gavana wa Benki Kuu (BoT), Prof. Emmanuel Tutuba, amesema serikali imetoa miongozo inayosimamia malipo ya kidijitali, ili kuongeza ujumuishaji wa kifedha kwa wananchi wengi zaidi.

Amesema mpango wa miaka 10 wa ujumuishaji wa kidijitali, inataka Tanzania ifikie malipo ya kidijitali, ili kuwafikia watu wengi, kurahisisha huduma za kifedha na kukuza uchumi.