Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu imeanzisha programu ya kuimarisha mfumo wa ufuatiliaji na tathmini kwa lengo la kusimamia kikamilifu utekelezaji wa miradi ya kilimo inayotengewa fedha na Serikali, ili kuhakikisha inaleta matokeo chanya katika sekta hiyo muhimu.
Akizungumza leo wakati wa uzinduzi wa programu hiyo mkoani Morogoro, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu), Dk. Jim James Yonazi amesema mpango huo umeambatana na mafunzo kwa wataalamu wa sekta ya kilimo nchini.
Amesema uzinduzi wa programu hiyo unalenga kuongeza ufanisi katika uzalishaji ambapo uzalishaji wa mazao ya chakula umeongezeka kutoka tani milioni 17 hadi tani milioni 22.
Dk. Yonazi amebainisha kuwa mfumo huo mpya utasaidia kutoa miongozo kwa wawekezaji katika sekta ya kilimo, kuhakikisha wanawekeza kwenye maeneo yenye tija na kwa kufuata vipaumbele vya taifa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Ufuatiliaji na Tathmini kutoka Wizara ya Kilimo, Joseph Kiraiya, amesema wataendelea kupitia programu mbalimbali za kimataifa na kufanya mapitio ya kisekta ili kuboresha miongozo ya ufuatiliaji na tathmini kwa miradi ya kilimo.
Naye Dk. Juma Makaranga, Mkuu wa Idara ya Uwekezaji, Ubia na Utafutaji Rasilimali kutoka Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo, amesema Serikali imeweka mpango kabambe wa mageuzi ya kilimo ili kuhakikisha wawekezaji wanaelekezwa kwenye maeneo sahihi na kuondokana na mfumo wa kilimo cha mazoea.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED