DCEA yateketeza ekari 614 za mashamba ya bangi, tisa wakamatwa

By Zanura Mollel , Nipashe
Published at 03:30 PM Jul 16 2025
DCEA yateketeza ekari 614 za mashamba ya bangi, tisa wakamatwa
Picha: Zanura Mollel
DCEA yateketeza ekari 614 za mashamba ya bangi, tisa wakamatwa

Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), kwa kushirikiana na Mamlaka ya Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA), imeteketeza ekari 614 za mashamba ya bangi na kusambaratisha kambi 72 za wakulima haramu wa zao hilo, huku watuhumiwa tisa wakikamatwa.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Aretas Lyimo, akizungumza na waandishi wa habari, amesema operesheni hiyo imefanyika katika ushoroba wa Hifadhi za Taifa za Mikumi na Nyerere, ambapo pia walikamata bangi kavu kilo 3,741.9 na kilo 1,706 za mbegu za bangi.

“Operesheni hii ni sehemu ya mapambano endelevu dhidi ya dawa za kulevya nchini. Tumeshuhudia mafanikio makubwa, ambapo mashamba ya bangi yamepungua na wakulima wake kuhamia maeneo ya mbali zaidi, jambo linaloonyesha mafanikio chanya ya juhudi zetu,” amesema Kamishna Lyimo.

Aidha, ameeleza kuwa DCEA itaendelea kushirikiana na taasisi za serikali na vyombo vya ulinzi na usalama kuhakikisha maeneo yote yanayotumika kwa kilimo haramu cha bangi yanadhibitiwa ipasavyo. Aliongeza kuwa elimu kwa jamii ni nguzo muhimu katika vita dhidi ya dawa za kulevya.

“Mamlaka imejipanga kuendelea kuhamasisha wananchi kufanya shughuli halali za kilimo ili kuepuka kuingia katika uhalifu wa kilimo na usambazaji wa dawa za kulevya,” ameongeza Lyimo.

Pia, Kamishna huyo amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na DCEA kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kukomesha kabisa biashara na matumizi ya dawa za kulevya nchini.

Kwa upande wake, Kamanda Mkuu Msaidizi wa Kikosi cha TANAPA, Moses Oko Onyango, ambaye alimwakilisha Mkuu wa Hifadhi ya Nyerere, ameema TANAPA ilishiriki operesheni hiyo baada ya kupokea taarifa kuhusu uwepo wa mashamba makubwa ya bangi katika eneo la Nyarutanga, karibu na mipaka ya Hifadhi za Mikumi na Nyerere.

“TANAPA inalinda uhifadhi endelevu wa maliasili. Hatutakubali maeneo ya hifadhi kutumika kwa shughuli haramu. Ushirikiano kati ya TANAPA na DCEA utaongeza nguvu katika kudhibiti uhalifu kwenye maeneo haya nyeti,” amesema Onyango.

Amesema kuwa kupitia Kitengo cha Mahusiano na Jamii, TANAPA iko tayari kushirikiana na DCEA kutoa elimu mashuleni na vijijini kuhusu madhara ya bangi na umuhimu wa kulinda mazingira.

Aidha, amesisitiza kuwa TANAPA itashirikiana kwa karibu na Mamlaka hiyo katika kufanya doria za pamoja katika maeneo yanayozunguka hifadhi kwa lengo la kudhibiti kabisa kilimo haramu cha bangi.