Serikali yaweka nia kila mwaka mtanzania ‘akamate’ mil 14/-

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 03:46 PM Jul 17 2025
Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo
Picha: Ibrahim Joseph
Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo

SERIKALI imeweka mkakati hadi kufikia 2050, pato la mtu mmoja mmoja liwe Dola 7,000 ambazo ni Sawa na sh milioni 14 kwa mwaka, huku Pato la Taifa liwe dola trilioni moja.

Waziri wa Mipango na Uwekezaji, Prof. Kitila Mkumbo, amesema hayo katika uzinduzi wa Dira ya Taifa 2050 iliyofanyika leo, Julai 17, 202, jijini Dodoma.

Amesema moja ya malengo ya serikali ni kuhakikisha kila mtanzania anapiga hatua katika mambo mbalimbali, ndio maana katika kipindi cha utengenezaji wa dira hiyo, maoni kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini yamekusanywa.

Amesisitiza kuwa hadi kufikia 2050, asilimia 90 ya watoto wafikie hatua sahihi za ukuaji, upatikanaji wa elimu bora na pia ifikapo mwaka huo, watanzania wote wawe na elimu ya kidato cha nne na asilimia 25 ngazi ya chuo kikuu. 

Mbali na hayo amesema zaidi ya asilimia 89 za huduma za serikali ziwe zinatolewea kwa njia ya TEHAMA ya huduma ziwafuate wananchi pale waliko.