Rais Samia aagiza maboresha Sheria ya Utekelezaji Dira 2050

By Renatha Msungu , Nipashe
Published at 03:16 PM Jul 17 2025
Rais Samia Suluhu Hassan
Picha: Ibrahim Joseph
Rais Samia Suluhu Hassan

RAIS Samia Suluhu Hassan, ameiagiza Tume ya Kurekebisha Sheria na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, kuanza kuandaa mapendekezo ya kuboresha Sheria ya uUtekelezaji wa Dira ya Taifa ya 2050.

Rais Samia amesema hayo leo, Julai 17, 2025, jijini Dodoma wakati wa hafla ya uzinduzi wa Dira ya Taifa 2050, iliyofanyika mkoani humo.

Amesema wakishirikiana katika utekelezaji wa dira hiyo, serikali itafikia malengo iliyojiwekea kwenye Dira ya Taifa ya 2050, iliyosheheni mambo mbalimbali.

"Nawapongeza sana waandaaji, lakini twende tukaitekeleze kwa vitendo na sio maneno peke yake," amesema Rais Samia.

Amefafanua kuwa kulingana na mabadiliko ya dunia ya sasa katika masuala ya kiuchumi, kila mmoja anakuja kivyake hivyo inapaswa kusimamiwa sera, ili tuweze kusonga mbele katika kukuza uchumi.

Rais Samia amesema kwa kutumia rasilimali za nchi, litajengwa taifa lililobora lenye mafanikio makubwa kama Dira ya Taifa ya 2050, ilivyoelekezwa.

Amefafanua zaidi ya kuwa Dira imeandliwa na kutolewa maoni na wananchi, hivyo inapaswa kutekelezwa, kwa sababu kunatabia ya kusemwa, lakini utekelezaji unakuwa mdogo.

"Maisha bora hujengwa kwa rasilimali pamoja na ustahimilivu hivyo twende kuitekeleza dira hiyo kwa weledi mkubwa," amesema Rais Samia.

Amesema katika kuandaa Dira ya 2050, wametafakari kwa kina na kuainisha mafanikio na changamoto, kwa kuzingatia hali halisi ya dunia ya leo.

Pia amesema pamoja na Makamu wa Rais, Dk.  Philip Mpango kuomba kupumnzika wadhifa huo, atapumnzika kiaina lakini jukumu la Dira ya Taifa ya 2050, ni jukumu lake.

Amesema Dk. Mpango ameshiriki pia katika uandaaji, pia ameizindua, hivyo ni jukumu lake.

"Nawapongeze sana waandaaji wa dira hii naamini itatekekezwa ipasavyo na tumeweza kutimiza mambo mbalimbali," amesema Rais Samia.

Amesema kipaumbele cha serikali ni kutumia rasilimali za nchi kujenga uchumi wa nchini, ingawa safari ndefu lakini tutafika tuendako.