BEKI wa kati wa Klabu ya Simba, Che Fondoh Malone, inaelezwa yupo mbioni kujiunga na Klabu ya USM Alger ya Algeria baada ya 'Wekunde wa Msimbazi', kumweka kwenye orodha ya wachezaji itakayoachana nao.
Inafahamika ripoti ya Kocha wa Simba, Fadlu Davids, imeeleza kocha huyo kutaka kusajiliwa beki wa kati na kuachwa Che Malone ambaye ameshindwa kumshawishi kuendelea kubaki.
Taarifa kutoka ndani ya klabu hiyo, imeeleza Che Malone tayari anajiandaa kuondoka ndani ya klabu hiyo na Waalgeria hao wameonesha nia ya kumtaka.
"Kuna timu kutoka Morocco na nyingine ya Algeria, zote zimeonesha nia ya kumtaka Che Malone, Simba inataka kumuuza na Waalgeria ambao ni USM Alger wao wapo 'serious' zaidi na kama mambo yataenda sawa, basi anaweza akajiunga nayo," alisema mtoa taarifa wetu.
Aidha, alienda mbali na kuweka wazi kocha Fadlu ameagiza winga wa timu hiyo, Joshua Mutale, aendelee kubaki klabuni hapo kwa kuwa yupo kwenye mipango yake.
Tayari Simba mpaka sasa imeachana na wachezaji Fabrice Ngoma na Valentine Nouma ambao wote wameagwa klabuni hapo kuwa hawatakuwa sehemu ya kikosi cha timu hiyo msimu ujao.
Aidha, uongozi wa klabu hiyo umeelezea upo kwenye kipindi cha usajili kuimarisha kikosi chao kwa ajili ya msimu ujao wa Ligi Kuu na mashindano ya kimataifa.
Meneja Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo, Ahmed Ally, aliliambia Nipashe jana kuwa mchakato wa usajili unaendelea kimya kimya na kwa umakini mkubwa.
"Wachezaji wote tunaowahitaji tunamalizana nao, wapo ambao tayari tumewasajili na muda ukifika tutaweka kila kitu wazi, usajili tunaufanya kwa umakini mkubwa, hatusajili kwa mihemko," alisema Ahmed.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED