Wachezaji Stars fiti kwa CHAN

By Adam Fungamwango , Nipashe
Published at 02:56 PM Jul 16 2025
news
Picha Mtandao
Wachezaji Stars fiti kwa CHAN

BAADA ya siku takriban 10 za mazoezi nchini Misri, wachezaji wa Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, sasa wako fiti kwenye utimamu wa mwili kuelekea michuano ya Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN), imeelezwa.

Akizungumza jana kutoka mji wa Ismailia, Misri, ambako kikosi hicho kimepiga kambi kujiandaa na fainali za CHAN, zinazotarajiwa kufanyika kwa ushirikiano wa nchini tatu za Afrika Mashariki, Tanzania, Kenya na Uganda, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Juma Mgunda, alisema suala la utimamu wa mwili wamelimaliza na kilichobaki ni kusonga mbele na mafunzo mengine.

"Tunashukuru kile ambacho tumekikusudia kinakwenda vizuri, tuko katika kazi ya kujenga utimamu wa mwili na inaonekana imekwenda vizuri, wachezaji tayari wako fiti, tunamalizia tu, lakini vile vyote ambavyo tumekusudia kuvifanya tumevifanya tumevitekeleza," alisema Mgunda.

Alisema kilichobaki sasa wanaingia kwenye hatua nyingine ambayo ni ya kiufundi na watamalizia eneo la saikolojia, huku wakieleza kuwa wachezaji wote waliopo kambini wana morali ya hali ya juu.

"Baada ya hapo tutakwenda kwenye suala la ufundi, halafu saikolojia, sisi makocha kazi yetu ni kuwatayarisha, halafu wao ndiyo watakaokwenda uwanjani kutuwakilisha.

"Niwatoe hofu tu Watanzania kuwa wachezaji wetu wana morali ya hali ya juu, wanajua wana deni kubwa, hivyo wameahidi kupambana hasa ikizingatiwa michuano ipo nchini, hasa kundi letu litacheza mechi zake hapa hapa," alisema.

Stars imepiga kambi kwenye mji wa Ismailia, ikifanya mazoezi yake katika viwanja vya Mercure, ikijiandaa na fainali hizo.

Inatarajia kufungua dimba, Agosti 2, mwaka huu, itakapomenyana dhidi ya Burkina Faso, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Jumla ya timu 19 zinashiriki fainali hizo zinazowashirikisha wachezaji wanaocheza ligi za nchini kwao, Stars ikiwa Kundi B na timu za Burkina Faso, Afrika ya Kati, Madagascar, na Mauritania.

Kundi A, lina timu za Angola, Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo, Kenya, Morocco na Zambia, huku Kundi C, likiundwa na timu za Algeria, Guinea, Niger, Afrika Kusini na Uganda.

Timu za Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Nigeria, Senegal na Sudan, zinaunda Kundi D, ambalo litatumia Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.