WAZIRI wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Zanzibar, Tabia Maulidi Mwita, amesema serikali zote mbili, ya Mapinduzi Zanzibar na ile ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, zimejiandaa vema kuelekea michuano ya Mataifa Afrika kwa wachezaji wa Ndani (CHAN), yanayoanza kutimua vumbi lake mapema Agosti mwaka huu.
Waziri Tabia alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari visiwani hapa jana, ambapo alisema kwa upande wa Zanzibar itakuwa inachezwa michezo ya Kundi D kuanzia Agosti 5, ambapo itashuhudiwa nchi za Senegal, Nigeria, DR Congo na Sudan zikimenyana vikali.
Alisema Uwanja wa New Amaan Complex, ndipo mechi hizo zitachezwa michezo hiyo na tayari Shirikisho la Soka Afrika (CAF), limekagua uwanja huo mara kadhaa na kutangaza kuwa umekidhi vigezo vya michezo ya kimataifa.
Alisema maeneo ya miundombinu yameboreshwa na kufikia vigezo vya CAF ikiwamo sehemu ya kufanyia mazoezi, pamoja na kuboresha huduma zote muhimu kama vile malazi, usafiri, ulinzi na huduma za afya zimeandaliwa kwa kiwango cha kimataifa.
Tabia alisema kamati maalum ya ndani ambayo imeteuliwa katika kuhakikisha inashughulikia masuala yote kwa maelekezo ya CAF inaendelea kufanya kazi ili kuhakikisha hakuna kinachoharibika katika maandalizi hayo kuelekea mashindano hayo.
'Kamati hii inafanya kazi yake vizuri kwa mujibu wa maelezo ya CAF, hadi kufikia sasa imefanyia kazi mambo yote ambayo inatakiwa kufanya, jambo ambalo ni faraja," alisema.
Aidha, alisema kuchezwa kwa mashindano hayo visiwani hapa, ni fursa ya kukuza uchumi, kuinua vijana, kutangaza utalii na kuimarisha mshikamano wa kitaifa.
Tabia alisema kupitia mashindano hayo pia yatasaidia kuongezeka kwa shughuli za kibiashara, ajira kwa vijana lakini pia kujitangaza kimataifa kupitia wageni watakaofika nchini kufuatilia michuano hiyo.
Hata hivyo, alisema Zanzibar ipo tayari si tu kwa ajili ya mechi bali pia kutoa uzoefu wa kipekee wa utalii na utamaduni kwa wageni ambao wataingia hapa nchini.
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED