Bwana harusi anayedaiwa kujiteka apanda tena kortini

By Grace Gurisha , Nipashe
Published at 12:52 PM Jan 08 2025
Bwana harusi anayedaiwa kujiteka apanda tena kortini.
Picha:Mtandao
Bwana harusi anayedaiwa kujiteka apanda tena kortini.

BWANA harusi, Vicent Massawe (36) aliyedaiwa kujiteka mwenyewe amepanda kizimbani kwa mara ya pili katika kesi ya wizi wa gari alilopewa kwa ajili ya kutumia kwenye harusi yake na upande wa mashtaka umedai upelelezi bado haujakamilika.

Massawe alifika jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu Beda Nyaki wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam akitokea nyumbani baada ya kutimiza masharti ya dhamana ya kuwa na wadhamini wawili na kuwasilisha mali isiyohamishika yenye thamani ya Shilingi milioni tisa.

Wakili wa Serikali Aron Titus, alidai kuwa kesi hiyo imeitwa kwa ajili ya kutajwa na upelelezi bado haujakamilika na kuomba tarehe nyingine ya kutajwa kwa shauri hilo.

Hakimu Nyaki aliahirisha kesi hiyo hadi Februari 12, 2025 kwa kutajwa.

Ilidaiwa kuwa Massawe ni mfanyabiashara na mkazi wa Kigamboni, katika shtaka la kwanza anatuhumiwa kuiba kama wakala. Inadaiwa Novemba 15, 2024 akiwa eneo la Kigamboni, Mkoa wa Dar es Salaam, aliiba gari hilo alilopewa na Silvester Beda kwa jili ya kulitumia kwenye harusi yake.

Inadaiwa gari hilo aliloazimwa alitakiwa kulirudiaha, lakini hakufanya hivyo, thamani yake ni Sh. milioni 15 mali ya Beda.

Katika shtaka la pili, Massawe siku hiyo hiyo na eneo hilo anatuhumiwa kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu Shilingi milioni tatu kutoka kwa Beda akiahidi kwamba atarudisha huku akijua si kweli.

Baada ya kusomewa mashtaka hayo alikana kuhusika na tuhuma hizo.

Awali, Massawe alidai kuwa gari ambalo anatuhumiwa kuliiba namba T 642 EGU Toyota Ractis ni la kwake na kwamba nyaraka zote anazo na kuiomba mahakama gari hilo liletwe mahakamani kama dhamana yake.

"Gari hili lililotajwa kwamba nimeliiba si kweli, gari ni langu, lakini taarifa iliyotolewa na kusambaa inadai gari sio langu, naomba gari liletwe kama dhamana yangu hapa mahakamani," alidai Massawe. 

Aliendelea kudai kwamba katika suala la dhamna hilo atalitimiza kwa sababu mali isiyohamishika yenye thamani ya Shilingi milioni tisa ipo. 

"Polisi walichelewa kunipa taarifa kuwa wananileta mahakamani, nikachelewa kutoa taarifa, lakini nimeshamwambia mke wangu yupo njiani anakuja hapa," alidai Massawe. 

"Bahati mbaya nilishatoa masharti ya dhamana kwamba mali isiyohamishika hiyo unaweza ukaitumia kama kielelezo," alisema Hakimu Nyaki. 

Hakimu Nyaki alimweleza mshtakiwa ili awe nje kwa dhamana anatakiwa awe na wadhamini wawili wenye vitambulisho vya NIDA watakaosaini bondi ya Shilingi milioni tano na pia atatakiwa kuwasilisha mahakamani fedha taslimu au mali isiyohamishika yenye thamani ya Shilingi milioni tisa.