Kili Stars kukamilisha ratiba

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 08:27 AM Jan 09 2025
Kili Stars kukamilisha ratiba.
Picha: Mtandao
Kili Stars kukamilisha ratiba.

TIMU ya Soka ya Tanzania Bara (Kilimanjaro Stars), inatarajia kuwakabili Burkina Faso katika mechi ya kukamilisha ratiba ya mashindano ya kuwania Kombe la Mapinduzi itakayochezwa leo kwenye Uwanja wa Gombani ulioko Kisiwani Pemba.

Kilimanjaro Stars tayari imeshaondolewa katika mashindano hayo baada ya kukubali kichapo cha pili mfululizo katika michuano hiyo ambayo mwaka huu inashirikisha timu za taifa.

Ushindi wa mabao 2-0 waliopata Kenya katika mechi iliyochezwa juzi usiku ilimaliza ndoto za Kilimanjaro Stars kuendelea katika michuano hiyo.

Katika mechi ya kwanza ya ufunguzi, Kilimanjaro Stars inayonolewa na Kocha Mkuu, Hamad Ally, ilifungwa bao 1-0 na wenyeji, Zanzibar (Zanzibar Heroes).

Mechi nyingine ya michuano hiyo ya kukamilisha hatua ya awali itakayochezwa leo itakuwa ni kati ya Zanzibar Heroes dhidi ya Burkina Faso.

Katika msimamo wa mashindano hayo, Kenya yenye pointi nne sawa na Burkina Faso iko kileleni ikifuatiwa na Zanzibar Heroes yenye pointi tatu.

Fainali ya mashindano hayo itafanyika Januari 13, mwaka huu kwa kushirikisha timu itakayomaliza katika nafasi ya kwanza dhidi ya nchi itakayokuwa iko kwenye nafasi ya pili.