WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mahmoud Thabit Kombo, amepongeza mafanikio yaliyofikiwa na Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC).
Akizungumza katika mahojiano na gazeti la China Daily mwishoni mwa wiki, Kombo alisisitiza kuwa ushirikiano baina ya China na Afrika si tu umekuza maendeleo ya kiuchumi na kijamii Tanzania, bali pia umeleta matokeo chanya kwa bara zima la Afrika.
Akitoa mfano wa kilimo cha soya kwa umuhimu wa maendeleo ya miundombinu kwa ajili ya kilimo cha kisasa, Kombo alisema kimeongeza tija na mauzo ya zao hilo nchini China, hivyo kunahitaji mitambo, maendeleo ya kisasa na uboreshaji wa miundombinu na haya ni maeneo yanayohusiana sana na ushirikiano na China.
“Kwa kushirikiana na China, Tanzania inaweza kuboresha hali ya usafiri na kupunguza gharama za usafirishaji, hivyo kuongeza ushindani wa soko la mazao ya kilimo,” alisema Kombo.
Balozi Kombo alizungumzia hatua 10 za ushirikiano zilizotangazwa kwenye mkutano wa FOCAC, ambazo zinashughulikia mahitaji muhimu ya Afrika, kama vile ustawi wa biashara, mnyororo wa viwanda, uunganishaji, kilimo, mambo ya afya, maisha ya watu na maendeleo ya kijani.
Kombo alisisitiza hatua ya ubia kwa maendeleo ya kijani ambayo ni moja ya hatua 10 za ushirikiano ambayo inawakilisha uwezo wa ushirikiano katika maendeleo ya kijani.
Alisema ana imani juu ya mustakabali wa ushirikiano wa maendeleo ya kijani kati ya China na Afrika.
“China inaongoza duniani kwa teknolojia na soko katika sekta ya betri. China na Tanzania zinaweza kufanya ushirikiano wa kina katika mnyororo wa viwanda vya betri ili kutoa fursa zaidi za ajira za ndani na kukuza mabadilishano ya kiufundi,” alisema.
Malengo Sita ya Maendeleo ya Kisasa na Hatua Kumi za Ubia zilizotangazwa na FOCAC 2024 zimetoa maarifa muhimu kwa ushirikiano wa Tanzania na China, hasa katika mambo ya mabadiliko ya kilimo na maendeleo ya kijani.
Ushirikiano wa Tanzania na China katika kukuza kilimo cha kisasa unaonesha umuhimu wa ushirikiano katika mnyororo wa viwanda. Kupitia maendeleo ya miundombinu na mitambo ya kilimo, tija na ushindani wa soko unaweza kuimarika.
Katika ushirikiano katika sekta ya betri, uunganishaji wa rasilimali za madini ya Tanzania na teknolojia ya China utakuza maendeleo ya sekta mpya ya nishati ya pande hizi mbili na kuleta fursa za ajira na uboreshaji wa viwanda Tanzania.
Imeandikwa na Ye Tianfi na Ning Yi
© 2025 IPPMEDIA.COM. ALL RIGHTS RESERVED