DED akaribisha wananchi wamhoji matumizi ya fedha

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 11:08 AM Jan 06 2025
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Khamis Katimba.
Picha: Mtandao
MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Khamis Katimba.

MKURUGENZI Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Khamis Katimba amewataka wananchi kufika ofisini kwake kuhoji matumizi ya fedha zinazokusanywa na kutumika kwenye halmashauri hiyo.

Alitoa msimamo huo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza katika kikao cha wadau wa maendeleo katika ukumbi wa halmashauri hiyo huku akisisitiza kuwa kila fedha inayokusanywa na kutumika ina maelezo yake.

Katimba alitoa kauli hiyo baada ya Mkuu wa Wilaya ya Malinyi, Sebastian Waryuba ambaye alikuwa mgeni rasmi katika kikao hicho, kumshauri kuwaeleza wananchi matumizi ya fedha zinazokusanywa na halmashauri hiyo.

Waryuba alianza kwa kumsifu mkurugenzi huyo kuongeza mapato na hata kukusanya asilimia 82 ya mapato ya ndani kwa miezi sita pekee (Julai – Desemba 2024).

"Nimefurahi kushuhudia kasi hii ya ukusanyaji mapato bila kutoana damu, mabadiliko haya yanaonesha kwamba huko tuendako tutafika salama.

"Mkurugenzi kasi hii isipungue, umeaminiwa na sisi tunakuamini kwa mikakati yako, simama imara na makusanyo yetu yapande zaidi lakini waone na matumizi yake," alisema Waryuba.

Akitoa ufafanuzi wa kauli hiyo ya Waryuba, Mkurugenzi Katimba alisema wananchi wakiona fedha zao zinafanya kazi gani, watahamasishana kulipa kodi kwa hiari.

"Mimi ninawaahidi, wao kazi yao ni kulipa kodi halafu waje waniwajibishe kwa matumizi ya fedha zao. Ninawaomba waendelee kulipa kodi ya serikali, lakini waje kuniwajibisha kwa matumizi ya fedha zao.

"Ofisi yangu ipo wazi kwa wote, hata akija mmoja mmoja ninaruhusu aje ofisini kwangu, aje aniulize 'umekusanya shilingi ngapi na umetumia shilingi ngapi?' Nitamueleza. Ofisi ipo wazi, ni ofisi ya wananchi wote, sisi ni dhamana tu," alisema.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Malinyi, Pius Mwelase alisema halmashauri hiyo ilikuwa haijawahi kukusanya mapato ya ndani asilimia 82 katika kipindi cha miezi sita pekee.

"Haijawahi kutokea mpaka Desemba kukusanya asilimia 82 kwenye halmashauri yetu, viporo vyote toka halmashauri yetu ianze tunavimaliza na kama kuna vingine semeni, sasa pesa ipo.

"Ubunifu aliokuja nao mkurugenzi wetu umeleta mabadiliko makubwa mno, tunajivunia na tunaamini bado tuna muda wa kutosha wa kukusanya fedha zingine nyingi kutokana na mikakati iliyopo kwa sasa," alisema. 

Akizungumza mwenendo wa makusanyo katika wasilisho lake, Ofisa Mipango wa Halmashauri hiyo, Richard Sanga alisema kuwa mpaka kukamilika kwa mwaka wa fedha 2023/24, halmashauri hiyo ilikusudia kukusanya Sh. bilioni 22.338 lakini ilifanikiwa kukusanya Sh. bilioni 20.445.

Alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2024/25, halmashauri hiyo iliidhinisha Sh. bilioni 26.790, mapato ya ndani yakiwa ni Sh. bilioni 4.334 na mpaka sasa - kwa miezi sita - mapato ya ndani, zimekusanywa Sh. bilioni 3.567.

Wakizungumza kwenye mjadala wa Rasimu ya Mpango wa Maendeleo na Bajeti ya Halmashauri hiyo kwa kipindi cha 2025/26, wadau wamegusia maeneo kadhaa wakitaka yafanyiwe kazi.

Mwananchi Omari Jumanne alisema halmashauri inapaswa kuandaa mpango madhubuti kuhakikisha wafugaji wanafuga kisasa na kuachana na ufugaji wa samaki wa kizamani.

"Samaki wanalipa hapa kwetu Malinyi, halmashauri isaidie sasa namna ya ufugaji kisasa, hili litasaidia kuongeza mapato," alisema.

Mwananchi mwingine Milard Ngapulile alishauri halmashauri kuandaa mfumo mzuri wa motisha kwa walimu na hata kulipa walimu wanaojitolea.

"Halmashauri itenge fedha kwa ajili ya walimu wanaojitolea na si kuwaachia mzigo huo walimu wakuu. Pia halmashauri inapaswa kuongeza motisha kwa walimu," alisema.

Neema Mgalagala alishauri kuwapo minada ya nyama choma ili wananchi wakajiliwaze baada ya kutafuta pesa.

"Tunatafuta fedha lakini hakuna pa kuzitumia, kwanini na sisi tusiwe na mnada wa mbuzi tukajipumzishe, tunahitaji kujiliwaza kwa kula vitu vizuri," alisema.

Rai ya mkurugenzi huyo kukaribisha wananchi kufuatilia matumizi ya kodi zao (makusanyo ya serikali) utaongeza uwajibikaji katika fedha za umma nchini ikiwa kutakuwa na mwamko huo kwa wananchi, pia wakurugenzi wengine kuruhusu wananchi kujua matumizi ya kodi zao.

Taarifa rasmi za kiserikali zinaonesha kupotea mabilioni ya shilingi ambayo yangetumika kuboresha miundombinu nchini.

Mtazamo huo wa fedha za umma kufanyiwa ubadhirifu, hata kusababisha pengo la ufanisi kwenye huduma za umma, unawasilishwa kupitia Uchambuzi wa Ripoti ya CAG kwa Mwaka 2022/23 uliofanywa na taasisi ya WAJIBU. 

Taasisi hiyo inayosimamiwa na CAG mstaafu Ludovick Utouh, mwanazuoni wa uhasibu, imebaini miamala mbalimbali yenye viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu wa fedha za umma, inayofikia Sh. trilioni 11.857 ndani ya miaka minne (2019/20 - 2022/23). 

Kiasi hicho kama kingeelekezwa kutatua uhaba wa miundombinu shuleni, kwa mfano, kingetosha kujenga vyumba vya madarasa mapya 592,850. 

Kwa mujibu wa Ofisi ya Rais - Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), chumba kimoja cha darasa kinajengwa kwa Sh. milioni 20 kikiwa na samani zake zote. 


Mwenendo wa viashiria vya rushwa, ubadhirifu na udanganyifu kuanzia mwaka 2019/20 hadi 2022/23. CHANZO: Ripoti ya Uwajibikaji ya taasisi ya WAJIBU.