173 watiwa mbaroni, wamo wa tuhuma za mafuta ya transfoma kukaangia chipsi

By Julieth Mkireri , Nipashe
Published at 11:38 AM Jan 06 2025
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase.

JESHI la Polisi Mkoa wa Pwani limewakamata watuhumiwa 173 wa makosa mbalimbali, yakiwamo ya usafirishaji nyara za serikali, dawa za kulevya, pombe haramu na wizi wa mifugo.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, Salim Morcase amesema watuhumiwa hao walikamatwa katika msako uliofanyika mwezi Desemba 2024 kwa lengo la kubaini, kuzuia na kutanzua uhalifu katika mkoa huo.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake mwishoni mwa wiki, Kamanda Morcase alisema kuwa katika msako huo, pia zilikamatwa nyaya za kopa Kg 3,687, mafuta ya diseli lita 3,547, mafuta ya transfoma lita 80 pombe ya moshi lita 86, bangi kilo tatu na gramu 120.5, mirungi Kg 7.04 na ng'ombe sita walioibwa.

Kuhusu nyaya za kopa, kamanda huyo alisema tayari watuhumiwa sita wamekamatwa huku wanne wengine wakishikiliwa na jeshi hilo wakihusishwa na lita 80 za mafuta ya transfoma zilizokamatwa.

Alisema ipo dhana imejengeka kuhusiana na mafuta ya transfoma kuwa ni mazito na yanapotumika kukaanga chipsi na samaki, hayaishi kwa haraka, jambo ambalo linachangia kutokoma wizi wa mafuta hayo.

"Mafuta haya yanadaiwa kutumika kukaangia chipsi au samaki kwa madai kwamba hayaishi haraka na ndio maana wanaendelea na wizi. Katika hili tunaahidi tutalikomesha, halitaendelea tena katika mkoa wetu," alionya.

Kwa upande wa nyara za serikali, Kamanda Morcase alisema watuhumiwa wanne walikamatwa wakiwa na meno ya tembo manane yanayokadiriwa kuwa na uzito wa Kg 67, vichwa vitano na miguu 53 ya mnyamapori aliyefahamika kwa jina la tohe na nyama ya swala vipande vinane vyenye uzito wa Kg 32.

Kamanda huyo pia alisema kuwa katika kipindi cha mwezi Desemba, kesi 125 zilifikishwa mahakamani. Kati yake, 47 zilipata mafanikio na kesi mbili kati ya tano za ukatili wa kijinsia zilipata ushindi.

Kamanda Morcase alisema katika kesi hizo za ukatili wa kijinsia, mtuhumiwa mmoja aliyekutwa na hatia alifungwa kifungo cha maisha gerezani kwa kosa la kubaka na kulawiti na mwingine alihukumiwa kifungo cha miaka 20 gerezani kwa kosa la unyanyasaji kingono.