Serikali yatoa mil. 75/- kuunga mkono ujenzi sekondari

By Sabato Kasika , Nipashe
Published at 02:07 PM Jan 06 2025
Serikali yachangia ujenzi wa sekondari Kijiji cha Muhoji
Picha: Mpigapicha Wetu
Serikali yachangia ujenzi wa sekondari Kijiji cha Muhoji

SERIKALI imatoa shilingi milioni 75 kuchangia ujenzi wa sekondari mpya ya Kijiji cha Muhoji, Jimbo la Musoma Vijijini, mkoani Mara, inayojengwa kwa nguvu za wananchi.

Shule hiyo inatarajiwa kuanza kuchukua wanafunzi wa kidato cha kwanza, mwezi huu kutoka vijiji vya jirani vikiwamo vya  Kaburabura, kata ya Bugoji na Saragana katika kata ya Nyambono.

Wanafunzi wengine wanaotarajiwa kusoma katika sekondari hiyo ni wale wanaotoka wilaya ya Bunda, hasa wanaoishi kwenye kitongoji jirani na Muhoji cha Kinyambwiga.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Prof. Sospeter Muhongo, amesema ujenzi wa miundombinu ya elimu kwenye sekondari hiyo unaendelea, ikiwamo maabara tatu za masomo ya sayansi, vyumba vya madarasa na nyumba za walimu.

"Serikali yetu imeanza kuchangia ujenzi wa sekondari hii kwa kutoa shilingi milioni 75. Tunaishukuru sana kwa mchango huo wa kusaidia jimbo letu kuwa na sekondari nyingi zaidi," amesema Prof. Muhongo.

"Majengo yaliyokamilishwa ni vyumba vitatu vya madarasa, ofisi moja, vyoo matundu nane ya wasichana na sita ya wavulana, chumba cha maktaba na chumba cha huduma ya kwanza," amesma.

Serikali yachangia ujenzi wa sekondari Kijiji cha Muhoji
Amesema, wakazi wa Muhoji wameamua kujenga sekondari yao, ili kutatua tatizo la umbali mrefu wanaotembea watoto wao, kwenda kupata elimu katika sekondari ya kata iliyopo kijijini Masinono.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Maregesi Mbai, amesema kuna umbali wa zaidi ya kilomita 10 kutoka Muhoji hadi Masinono na kwamba uamuzi wao wa kujenga sekondari ya kijiji, utaondoa kikwazo hicho.

"Tumeungana kusomba mawe, mchanga, maji na kutoa fedha taslim katika kazi hii hadi tumefikia hapo tulipo, huku mbunge naye akichangia fedha zake, fedha za mfuko wa jimbo nazo zimetumika," amesema Mbai.