Askofu Shoo ataka mafunzo ya unyago, jando kunusuru ndoa kuvunjika

By Godfrey Mushi , Nipashe
Published at 04:35 PM Jul 01 2024
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Frederick Shoo.
Picha: Maktaba
Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Frederick Shoo.

ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini, Dk. Frederick Shoo ameitaka serikali, viongozi wa dini, mila na malezi kurejesha mafunzo ya jando na unyago katika jamii ili kunusuru ndoa nyingi kuvunjika nchini.

Dk. Shoo alitoa rai hiyo mwishoni mwa wiki iliyopita wakati akizungumza katika Mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro na wajumbe 390 wa Idara ya Malezi ya Dayosisi hiyo.

Alisema viongozi hao wanapaswa kurudi kuwafunda vijana, kuwaandaa  kuchukua majukumu ya kuwa mume na mke ili kunusuru ndoa nyingi kuvunjika. 

“Pale misingi inapotetereka, hakika matokeo yake tunayaona katika kuvunjika kwa ndoa, kuharibika kwa ndoa. Maana yake ni nini? vijana wetu hawajaandaliwa, hawajalelewa katika kuchukua majukumu. Hawaelewi maana ya ndoa ni nini, hawaelewi maana ya kuishi mume na mke, wajibu wao ni kitu gani,” alisema na kusisitiza kuwa: 

“Tunapoona hakuna umuhimu wa kuwaandaa vizuri vijana hawa, basi matokeo yake, ndio tunayoyashuhudia sasa. Kwa hiyo mimi niseme, utumike muda wa kutosha, viongozi wa dini, viongozi wa malezi katika jamii kwa ujumla, hata wale wa kimila iwafundishe vijana wetu, tuwaandae vizuri katika kuchukua majukumu ya kuwa mume na mke.” 

Askofu Dk. Shoo, alifafanuwa kuwa mafunzo hayo  lengo lake ni kuwafundisha vijana jukumu la kubeba wajibu wao kama mume, mke na mzazi. 

“Nafikiri hilo ndilo linalohitajika kufanyika na tusifikirie tu kwamba tunaweza kufanya kwa akili zetu. Ndio kuna akili na maarifa mengi kutokana na uzoefu na taaluma, pia kuna jambo la kumcha Mungu,” alisema. 

Kiongozi huyo wa kiroho, alisema ndoa na unyumba vikitunzwa, watoto watalelewa vizuri na kutokea jamii yenye afya. 

“ Sasa hivi tunazungumzia tatizo la afya ya akili lakini ukiangalia msingi wake ni watu wameacha hofu ya Mungu. Msingi wake watu wameacha kutunzana, kuleana mpaka inafikia mtu anaharibikiwa, anapatwa na msongo wa mawazo. Watu wanapata mambo mazito ambayo hawana mtu wa kuwasaidia, kwa hiyo tushirikiane wote kujenga familia imara,” alisema. 

Hivi karibuni, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mipango na Uwekezaji), Profesa Kitila Mkumbo akizungumzia kuhusu masuala ya talaka, wakati akiwasilisha taarifa ya hali ya uchumi wa taifa kwa mwaka 2023 na Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa Mwaka wa Fedha 2024/2025 Bungeni Jijini Dodoma alisema: 

Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA), umesajili hati za talaka 866 mwaka 2023, ikilinganishwa na hati za talaka 447 zilizosajiliwa mwaka 2022. 

Kwa mujibu wa RITA, umesajili hati za viapo vya ndoa 45, 455, ikilinganishwa na hati za viapo vya ndoa 51,011 mwaka 2022. 

Awali, Katibu wa Idara ya Malezi wa Dayosisi hiyo, Mchungaji Faustina Mmari Kahwa, alisema mkutano huo mkuu wa 41 wa idara hiyo, uliketi kutoa taarifa ya kazi zilizofanywa kwa muda wa miaka minane. 

Kwa mujibu wa Mchungaji Kahwa, wajumbe wa mkutano huo wanaotoka katika sharika zote 173 za Dayosisi hiyo ya Kaskazini.