Mhagama: Serikali itaendelea kuwatumikia wananchi kwa weledi

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 08:03 PM Jul 03 2024
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama akipata maelekezo.
Picha: Maulid Mmbaga
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama akipata maelekezo.

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge na Uratibu Jenista Mhagama, amesema serikali itaendelea kuwahudumia wananchi na kuhakikisha wanapata huduma bora na kwa wakati unaotakiwa kwa lengo la kuwaletea maendeleo na taifa kwa ujumla.

Amesema hayo  leo wakati alipotembelea banda jumuishi la Ofisi ya Waziri Mkuu na Taasisi zilizopo chini yake katika maonesho ya 48 ya Biashara ya Kimataifa (SABASABA) ili kujionea jinsi watumishi wa ofisi hiyo wanavyotoa huduma kwa wananchi na wadau kwa ujumla.

Akiwa katika banda hilo Waziri Mhagama ameonyesha kufurahishwa na huduma zinazoendelea kutolewa pamoja na elimu juu ya shughuli zinazotekelezwa na ofisi yake huku akiwasihi watumishi wa ofisi hiyo kuzingatia weledi, ufanisi, huduma nzuri na kuzingatia misingi ya utumishi wa umma wawapo katika utekelezaji wa majukumu hayo. 

“Tuendelee kuwahudumia wananchi, na tumeamua kuwafikia kwa karibu kupitia maonesho haya hivyo tunawakaribisha wananchi wote kuendelea kutembelea banda la ofisi ya waziri mkuu, tumejiandaa vizuri kuwahudumia,” amesema Mhagama.

Ameongeza kwa kueleza juhudi za serikali chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha diplomasia na sekta zote nchini katika kuhakikisha taifa linajipatia kimaendeleo.

“Rais ameendelea kuwa kinara na mpambanaji kwa ajili ya wananchi wote na niwahakikishie kuwa mama yupo kazini na ameendelea kusimamia sekta zote na kuhakikisha miradi yote ya kimkakati inaimarika ili kujiletea maendeleo yetu,” amesema Mhagama.