Wivu wa mapenzi, imani za kishirikina, kulipiza visasi chanzo cha mauaji Katavi

By Neema Hussein , Nipashe
Published at 01:44 PM Jul 06 2024
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani, akionyesha baadhi ya vifaa vinavyodhaniwa kuwa vya wizi.
PICHA Neema Hussein
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, Kaster Ngonyani, akionyesha baadhi ya vifaa vinavyodhaniwa kuwa vya wizi.

Jeshi la Polisi mkoa wa Katavi linawashikilia watuhumiwa 74 kwa kujihusisha na matukio mbalimbali ya uhalifu, kati yao; watuhumiwa 12 wanadaiwa kujihusisha na matukio ya mauaji yaliotokea kwa nyakati tofauti mkoani Katavi.

Akitoa taarifa ya utendaji kazi wa Jeshi la Polisi kwa mwezi Juni 2024 Kamanda wa Jeshi la Polisi mkoani humo, RPC Kaster Ngonyani amesema matukio mengi ya mauaji mkoani Katavi yanatokana na imani za kishirikina, wivu wa mapenzi na watu kulipizana visasi.

Mbali na hilo pia Kamanda Ngonyani amesema tayari wanawashikilia watuhumiwa 30 ambao wanajihusisha na wizi wa madirisha ya ‘aluminum’ katika shule mbalimbali ndani ya Manispaa ya Mpanda pamoja na unyang'anyi wa kutumia slaha.

Aidha kamanda huyo ametoa rai kwa jamii, kuacha mara moja tabia ya kujichukulia sheria mkononi, ikiwemo ndugu kuuwana wenyewe kwa wenyewe.

Kamanda Ngonyani amesema watuhumiwa wote wanaendelea kuhojiwa na mara baada ya upelelezi kukamilika watafikishwa mahakamani kujibu tuhuma zinazowakabili.