Katibu Mkuu aagiza WMA kutekeleza maono ya Rais

By Mwandishi Wetu , Nipashe
Published at 07:09 AM Oct 05 2024
KATIBU Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Hashil Abdallah.
Picha:Mtandao
KATIBU Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Hashil Abdallah.

KATIBU Mkuu Wizara ya Viwanda na Biashara, Dk. Hashil Abdallah, ameitaka Menejimenti ya Wakala wa Vipimo (WMA) kutekeleza maono ya Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuzingatia utendaji kazi wenye weledi, ubora na viwango ili kupata matokeo chanya katika sekta ya biashara nchini.

Dk. Abdallah aliyasema hayo juzi Kibaha mkoani Pwani baada ya kufungua rasmi kikao cha menejimenti ya WMA, kukabidhi magari ili kuboresha utendaji kazi na kuzindua Jarida Maalum la Wakala lenye lengo la kupanua wigo wa uelimishaji na uhabarishaji umma kuhusu WMA.

“Lengo kubwa la kikao chetu ni kukumbushana wajibu na dhamira nzima ya majukumu yetu ambayo yanatakiwa yaakisi maelekezo na miongozo ya Rais Dk. Samia Suluhu Hassan katika suala zima la kuwezesha ufanyaji biashara ndani ya nchi yetu,” alisema.

Ili kuhakikisha maono ya Rais yanafikiwa, Dk. Abdallah aliitaka WMA kuzingatia  utii wa sheria, miongozo na kanuni mbalimbali zilizopo kwa kuongeza uadilifu na weledi kazini.

Pia aliwataka kufanya kazi kwa ushirikiano kama timu moja na kuwa na kauli moja baina ya bodi, mkuu wa wakala, menejimenti, viongozi wa mikoa na wafanyakazi wote kwa lengo la kupata matokeo chanya katika kazi.

Vilevile, aliielekeza Menejimenti kuondoa urasimu wa aina yoyote katika utendaji kazi huku akisisitiza kwamba jarida alilozindua pamoja na kutoa habari mbalimbali za wakala, litumike kama nyenzo ya utoaji taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na wadau wa WMA hususani katika ufanyaji biashara.

Katibu Mkuu alisisitiza uongozi wa WMA kuzingatia yaliyomo katika Mkataba wa Huduma kwa Mteja, ambao unaelekeza kutoa huduma bora na kwa wakati.

Katika hatua nyingine, Dk. Abdallah alimpongeza na kumshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuboresha mazingira ya utendaji kazi kwa sekta mbalimbali za umma na kwa muktadha huo kwa WMA na ametoa magari 10 kwa wakala hiyo ili kuboresha utendaji kazi.

“Leo (juzi) nimekabidhi magari mawili kwa WMA na mengine manane yako kwenye mchakato na tutayakabidhi mara moja utakapokamilika. Kwa hili, tuendelee kumshukuru sana Mheshimiwa Rais,” alisema.

Akizungumza kwa niaba ya menejimenti nzima, Ofisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla, alisema watatekeleza maelekezo yote yaliyotolewa na Katibu Mkuu.

Kuhusu majukumu ya WMA ambayo ndiyo hasa yaliyotolewa maelekezo kuongeza nguvu, Kihulla alisema ni pamoja na uhakiki wa vipimo, ukaguzi wa vipimo na ukaguzi wa bidhaa zilizofungashwa kwa lengo la kukuza uchumi katika sekta mbalimbali.

“Lengo ni kukuza uchumi katika sekta mbalimbali lakini pia kusaidia wananchi wanaonunua bidhaa mbalimbali zinazozalishwa nchini na zinazotoka nje ya nchi, ziwe katika uzito sahihi, ujazo sahihi, urefu sahihi pamoja na namba yaani idadi sahihi,” alisema.

Kuhusu magari waliyopokea, Kihulla aliishukuru wizara na kukiri kuwa yatapunguza changamoto iliyopo lakini akaomba wakala iendelee kufikiriwa kupatiwa mengine zaidi pamoja na vitendea kazi vingine mbalimbali ili kuboresha zaidi utoaji huduma kwa wananchi.

Kikao hicho cha menejimenti ya WMA ni utaratibu wa kawaida ambao wakala imejiwekea kwa kukutana kila robo ya mwaka wa fedha kujadili maendeleo ya utendaji kazi na namna ya kuboresha zaidi. 

Kikao hicho cha siku tatu kilichoanza Oktoba 2, mwaka huu, kimejumuisha menejimenti kuu kutoka makao makuu na mameneja wa mikoa yote Tanzania Bara.