Watoto msikae kimya mnapofanyiwa ukatili

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 12:19 PM Jul 06 2024
Asma Mwinyi, (Wa pili kushoto) Mkurugenzi wa Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation (AMF), akimkabidhi mfano wa taulo kwaajili ya wanafunzi wa kike Omary Mwanga, (Wa pili kulia) Katibu Tawala Wilaya ya Mkuranga.
Picha: Maulid Mmbaga
Asma Mwinyi, (Wa pili kushoto) Mkurugenzi wa Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation (AMF), akimkabidhi mfano wa taulo kwaajili ya wanafunzi wa kike Omary Mwanga, (Wa pili kulia) Katibu Tawala Wilaya ya Mkuranga.

OFISA Ustawi wa Jamii Wilaya ya Mkuranga Amina Aloyce amewasisitiza wanafunzi katika wilaya hiyo pamoja na Tanzania kwa ujumla kuhakikisha hawafichi matukio ya ukatili wa kijinsia wanayofanyiwa kuepuka kukuza tatizo hilo.

Ametoa rai hiyo Mkuranga mkoani Pwani, wakati Taasisi ya Asma Mwinyi Foundation (AMF) ilipokuwa ikigawa msaada wa taulo za kike kwa wanafunzi 842 wa Shule ya Sekondari ya Ali Hassan Mwinyi. Katika kuadhimisha siku ya Kiswahili nchini.

Amesema kumekuwa na aina zaidi ya tatu za ukatili wa kijinsia ambazo watoto kwa ujumla wamekuwa wakifanyiwa katika mazingira tofauti lakini kumekuwa na tatizo kwa baadhi yao kushindwa kuyawasilisha kwa walezi wao baada ya kufanyiwa.

"Tunaomba wazazi, wananchi, na wanahabari waeendelee kutusaidia kupaza sauti katika kukemea ukatili, kwa watoto wetu, kila mmoja ajue kuwa anajukumu la kumlinda mtoto," amesisitiza Amina.

Mkurugenzi wa AMF, Asma Mwinyi, amesema dhumuni la kutoa taulo hizo ni ili kumuwezesha mwanafunzi kuwa na furaha na kuendelea kuhudhuria darasani pasipo kuwa na shaka yoyote, hasa akiwa kipindi cha hedhi, ikiwa ni muendelezo wa kampani yake ya (Nisitiri Nisifenzeheke).

"Jitihada hizi kwa kiasi kikubwa ni ili kuunga mkono mkakati wa serikali katika kutoa elimu bora kwa wanafunzi bila kukutana na changamoto yoyote inayoweza kuwafanya washindwe kuhudhurua masomo yao," amesema Asma.

Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkuranga, Omary Mwanga, amesema jitihada hizo zinafanyika kwa kuzingatia umuhimu wa wanawake, na kwamba hiyo ni katika kuwatengenezea mazingira mazuri watoto kwa mustakabali wa maendeleo yao, jamii na taifa.

Amesema serikali pia inafanya jitihada kubwa kushirikiana na wadau wa maendelea kama taasisi hiyo katika kuhakikisha mazingira rafiki kwa wanafunzi, kwakuwa siku za nyuma kulionekana kuwa hedhi ni tatizo linalosababisha wanafunzi kutohudhuria darasani.

"Nyinyi jukumu lenu kwa serikali na taasisi hizi zinazowasaidia ni kusoma ipasavyo na kwa bidii mfaulu ili muendelee kuwashawishi, mtakapofeli mtakuwa mumewaangusha, niwasisitize kwamba matarajio yetu kutoka kwenu ni kufaulu mitihani yenu kwa faida yenu, familia, jamii na taifa kwa ujumla," amesema Mwanga.

Ameongeza kuwa masuala ya unyanyasaji wa kijinsia yameendelea kufanyika, akisisitiza maofisa wa serikali, wanafunzi, walimu na wanzani kuunga mkono jitihada za kupinga ukatili kwa jamii.

"Ukiona kwamba kuna jambo linafanyika ambalo unahisi litaathiri ufauli wako iwe umefanyiwa na kaka, mjomba shangazi usikae kimya semeji kwasababu sisi viongozi tuko kwaajili ya kuwasaidia mujiamini toa taarifa tuweze kukusaidia.

"Kuna wengine anashinda kumuambia mwalimu ila rafiki yake anaweza kumuambia, sasa wewe rafiki ulieambiwa msaidie mwenzako kufikisha hilo kwa mwalimu ili asaidiwe," amesisitiza Mwanga.