Safari za ATCL sasa rasmi Oman

By Joseph Mwendapole , Nipashe
Published at 10:00 AM Jun 28 2024
Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).
Picha: Maktaba.
Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL).

KATIKA kutanua wigo wa safari zake za kimataifa, Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), iko kwenye maandalizi ya kuanzisha safari za moja kwa moja kuelekea Muscat nchini Oman.

Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Ndege Tanzania (ATCL), Mhandisi Ladislaus Matindi, alipokutana na Balozi wa Oman nchini, Saud bin Hilal Alshaidani, juzi katika Ofisi za Ubalozi zilizopo jijini Dar es Salaam. 

"Taratibu za kufungua kituo nchini Oman zimeanza ambapo Air Tanzania tumeshampata wakala mkuu wa mauzo ya tiketi zake nchini Oman (General Sales Agent), tumeteua msimamizi wa kituo hicho," amesema Mhandisi Matindi.

Ameongeza kuwa kwa sasa hatua iliyofikiwa ni kukamilisha uandaaji wa timu ya marubani, ndege itakayotumika pamoja mpangilio wa safari.

Balozi wa Oman nchini Tanzania, Saud bin Hilal Alshaidani, amesema mazungumzo yake na Air Tanzania yamekuwa na tija na wamejadili fursa zilizopo kwa kutumia ndege za abiria na mizigo.

"Kwa idadi kubwa ya raia wa Oman waliopo hapa nchini, biashara kati ya nchi hizi mbili ikiendelea kukua ni matarajio yangu kuwa Air Tanzania itanufaika na fursa hii bila kuwa na mshindani," amesema Balozi Alshaidani.

 “Tunaweza kujikita kwenye usafirishaji wa aina tatu tu za matunda zenye uhitaji mkubwa nchini Oman, maembe, nanasi na parachichi. Hii itanufaisha pande zote, wafanyabiashara wa Tanzania na Oman,” amesema.

Kwa sasa Air Tanzania inafanya safari za ndani ya nchi kwa zaidi ya vituo 10. Kwa safari za kikanda na kimataifa ina safari za Dubai (UAE), Mumbai (India), Guangzhou (China), Bujumbura (Burundi), Entebbe (Uganda), Hahaya (Comoro), Harare (Zimbabwe), Lusaka na Ndola (Zambia), Nairobi (Kenya) na Lubumbashi (Congo).

Kwa Tanzania ATCL imekuwa ikifanya safari zake kati ya Dar es Salaam kwenda mikoa ya Dodoma, Mwanza, Mbeya, Kilimanjaro, Arusha, Songea, Katavi, Zanzibar, Mtwara, Tabora na Kigoma.