Aweso awa mbogo, aagiza vigogo DAWASA kusimamishwa kazi

By Frank Monyo , Nipashe
Published at 11:59 AM Jul 02 2024
WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso.

WAZIRI wa Maji, Jumaa Aweso ameiagiza Bodi ya Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA), kuwasimamisha kazi vigogo wawili wa mamlaka hiyo, akiwamo Kaimu Ofisa Mtendaji Mkuu, Kiula Kingu ili kupisha uchunguzi.

Mwingine ni Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji wa DAWASA, Shaban Mkwanywe.

Ameagiza mamlaka hiyo kuwa chini ya Wizara ya Maji kwa muda mpaka ufumbuzi utakapopatikana.
 Alitoa agizo hilo jana kwenye ofisi za makao makuu ya DAWASA, Ubungo mkoani Dar es Salaam, baada ya kufanya ziara ya kushtukiza katika maeneo ya Chuo Kikuu cha Ardhi, Mbezi, Mshikamano na Tegeta A ambako kuna matangi ya maji.

Viongozi hao wamesimamishwa kutokana na ripoti iliyotokana na ziara ya Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Mhandisi Mwajuma Waziri, iliyobaini utendaji usioridhisha ndani ya taasisi hiyo ikiwamo kutofanyia matengenezo miundombinu chakavu ya usafirishaji maji kutoka kwenye vyanzo hadi kwenye matangi ya kuhifadhia maji.

 "Mtendaji Mkuu (Kiula) changamoto hii ya uzalishaji wa maji unaifahamu na nilishakupa maagizo ya kuchukua hatua tena nilikutajia majina, lakini hujachukua hatua, matokeo yake mnafanya kazi kirafiki 'kishikaji.” 

“Nilikuagiza ukaonane na katibu mkuu kwa zaidi ya mara tatu hukuwahi kufanya hivyo na katibu mkuu alifanya ziara hapa viongozi hamkuonekana kirahisi tu," alisisitiza.

Aidha, alisema kushindwa kufanya matengenezo wakati kila mahitaji yapo, ni hujuma zinazolenga kuiharibia serikali kwa wananchi wake wanaolalamikia maji kila uchwao.

"Lazima nichukue hatua, bodi nawaomba msimamisheni Mhandisi Shaban (Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji wa DAWASA) na tutafuatilia kwanini uzalishaji anaosema hauakisi kwenye matangi ya kuhifadhia maji. Kama maji mtoni yapo na umeme upo kwanini maji kwenye matangi hakuna na watu hawapati maji," alihoji Aweso.

"Bodi naomba pia msimamisheni Mtendaji Mkuu kwa kushindwa kutekeleza wajibu wake, nilimwagiza lakini yupo kimya anafanya kazi kindugu wanashindwa kutambua tunawalipa mshahara kwa kodi za watanzania," alisema. 

Aweso alimuhoji Mkurugenzi wa Uzalishaji na Usambazaji Maji wa DAWASA, Shaban Mkwanywe mbele ya waandishi wa habari na mahojiano hayo yalikuwa hivi:

Aweso: Waeleze wenzako, tumefika Chuo Kikuu Ardhi, tangi la lita milioni 40, maji yapo?

Mkwanye: Hayakuwapo

Aweso: Tumetoka pale, tumekwenda kwenye ‘flow meter, flow inhalers’ zinafanya kazi?

Mkwanye: Hazifanyi kazi Mheshimiwa.

Aweso: Lakini tumemkuta mtu anaandika kwenye kitabu juu ya uzalishaji maji, anaandika data kutoka wapi wakati ‘flow meter’ hazifanyi kazi?

Mkwanye: Sielewi Mheshimiwa.

Aweso: Tumeenda Kibamba, tangi lina lita ngapi?

Mkwanye: Milioni 10

Aweso: Haya embu tuambie ndani kuna lita ngapi pale?

Mkwanye: Kulikuwa hakuna maji.

Aweso: Kwa ukali; Lita ngapi sema!?

Mkwanye: Ziro.

Aweso: Sasa kama maji hakuna, malalamiko yatakuwepo, hayatakuwepo?

Mkwanye: Yatakuwapo.

Aweso: Nani anahusika na uzalishaji?

Mkwanye: Ni mimi Mheshimiwa.

Aweso: Ili tuwe na uzalishaji tunahitaji mambo mawili, la kwanza lazima tuwe na maji kwenye chanzo kwa maana ya mito, maji yapo, hayapo?

Mkwanye: Yapo Mheshimiwa.

Alisisitiza kuwa serikali imewekeza fedha kwenye utekelezaji wa miradi ya maji Dar es Salaam, Ruvu Juu na Chini ili watu wapate maji.

“Jukumu la DAWASA watu wapatiwe majisafi na salama, umeme upo, maji yapo, hatuna kisingizio, Kwanini maji kwenye matangi hayapo?  Kwanini nisiwaombe polisi kukukamata kwa sababu umeme upo, maji yapo, kwanini wewe na timu yako nisiwaweke ndani?” Alihoji. 

Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Jenerali mstaafu, Davis Mwamunyange, alisema katika ziara waliyofanya maeneo machache wamepata picha halisi.

"Hali ya utoaji huduma ya maji kwakweli ni mbaya na ziara ilikuwa ya kushtukiza na aliyofanya katibu mkuu ilikuwa ya kushtukiza zinafaa zaidi kuliko zile rasmi kwakuwa watendaji wanakuwa wamejiandaa,” alisema Mwamunyange na kuongeza;

“Mimi sikutarajia na wajumbe wenzangu wa bodi tutakuta hali hiyo imetushtua. Ni jambo ambalo hatukulitarajia na hatua za haraka zinapaswa kuchukuliwa," alisema.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mwajuma Waziri, alisema uwajibikaji wa watendaji wa DAWASA hauridhishi huku akieleza maji yanayopotea ni mengi.

Ziara ya Aweso imefanyika baada ya ziara ya Katibu Mkuu wa Maji aliyoifanya kwa siku mbili kujionea utendaji kazi wa DAWASA na hali ya upatikanaji wa maji.

Aidha, alibaini kuwapo uzembe aliouwasilisha kwa waziri ikiwamo miundombinu ya maji kuwa chakavu, maji kupotea bila usimamizi, watendaji wa DAWASA wa ngazi za chini kutopewa stahiki zao muhimu na kusababisha kufanya kazi bila hamasa nzuri na hata kuwajibu vibaya wateja.