Barabara Rangi Tatu Mkuranga kutanuliwa

By Maulid Mmbaga , Nipashe
Published at 02:21 PM Jan 01 2025
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega.
pigapicha Wetu
Waziri wa Ujenzi Abdallah Ulega.

WAZIRI wa Ujenzi Abdallah Ulega amesema tayari wameshaanza mchakato wa upanuzi wa barabara kutoka Rangi Tatu hadi Mkuranga, baada ya kupata kibali kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan.

Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika jana wilayani Mkuranga mkoani Pwani, Ulega amesema upanuzi wa barabara hiyo umekubalika ili kuondoa msongamano mkubwa unaosababisha adha kwa wananchi wa Mkuranga, Kibiti, Rufiji na maeneo yote ya ukanda wa Kusini.

"Rais Samia amenipa kibali cha upanuzi wa barabara hii na kuniruhusu kutangaza tenda ya kazi hiyo. Tayari fedha zipo, na tunakwenda kuitanua barabara kutoka Rangi Tatu kuja mpaka Kongowe na kuendelea. TANROADS na TARURA Mkoa wa Pwani wapo tayari kuanza kazi," amesema Ulega.

Ulega amebainisha kuwa msongamano katika barabara ya Rangi Tatu (Mkoani Dar es Salaam hadi Kongowe umekuwa kikwazo kikubwa kwa maendeleo ya ukanda wa Kusini hivyo maagizo ya Rais Samia yanaenda kuleta tumaini endelevu kwa watumiaji wa barabara hiyo kutoka Mkuranga.

1


"Maendeleo yetu yanachelewa sana kwa muda tunaotumia katika eneo hili. Mtu anaweza kuondoka Mkamba mapema, lakini akifika Mwandege kuelekea Kongowe, Dar es Salaam, anapoteza muda wa saa mbili au tatu. Hili lazima lifike mwisho," amesisitiza.

Kwa mujibu wa Waziri Ulega, Rais Samia alimpa jukumu la kuhakikisha tatizo hili linatatuliwa kwa haraka.

"Rais Samia amenituma, amenielekeza na kuniambia, 'Uliomba jambo hili, leo kijana wangu Ulega ninakukabidhi mfupa huo kamalizane nao mwenyewe sasa,' ameeleza Ulega.