Biteko akerwa makandarasi wanaodai rushwa

By Paul Mabeja , Nipashe
Published at 09:47 AM Aug 22 2024
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko
Picha:Mpigapicha Wetu
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko amekerwa na tabia ya baadhi ya makandarasi wanaogeuka kuwa madalali wa kupiga dili na kudai rushwa kwa wananchi wakati wa kupeleka umeme kwenye vitongoji.

Biteko alisema hayo baada ya kushuhudia utiaji saini mikataba ya makandarasi 25 na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambao umelenga kupeleka nishati ya umeme katika vitongoji 15 kwa kila jimbo isipokuwa majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema kumekuwapo na taarifa kuwa baadhi ya makandarasi wakati wa kutekeleza miradi ya kupeleka umeme vijijini waligeuka kuwa madalali wa kupiga dili na kuomba rushwa kwa wananchi.

“Kuna maeneo mengine unakuta makandarasi na watu wao wamegeuka kuwa madalali wa kupiga dili kwa wananchi. Mkandarasi anajua hapa nitapeleka umeme, lakini ama kibarua ama fundi wanapita kwa wananchi wanawaomba fedha.”

“Ziko taarifa za makandarasi wetu wanapoenda kupeleka umeme vijijini wanao waomba fedha wananchi kwa fedha ambayo serikali imeshaitoa, kwamba ili nikusogezee nguzo kwako nipe kiasi hiki.”

“Nataka niwaombe makandarasi wa REA, nikipata taarifa juu ya mkandarasi yeyote ambaye badala ya kufanya kazi ya kupeleka umeme ameingia kwenye dili la kutafuta fedha kidogo kwa Watanzania masikini ambao serikali imejinyima ili kuwapelekea umeme mimi sitashughulika na mkandarasi nitashughulika na wewe mtendaji wa REA kwa sababu lazima tufike mahali Watanzania wajue hii ni haki yao wanastahili kupata bila watu kutishwa na kuombwa rushwa, lazima tuwe watendaji wa watanzania ambao tuko daraja la juu tunaostahili kupata hizi huduma.”

Pia, aliitaka REA kuendelea kusimamia makandarasi bila kuwaonea ili utekelezaji wa miradi ya umeme iende kwa kasi na kuhakikisha inafanya malipo kwa wakati kwa makandarasi ili aendelee kufanyakazi.

“Tukicheleweshana, tukaanza kufanya urasimu, mtu ameleta certificate mtu mmoja mahali fulani lazima mwonane ndio ulipwe hilo jambo kwanza linakera na kuudhi maana yeye ni mfanyabiashara na hakuja hapa kupiga picha.”

Alisema fedha zilizotengwa kutekeleza mradi huo ni nyingi na itakuwa ajabu zikija kufanyiwa tathmini wakute maelezo badala ya mradi kutekelezwa.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa REA, Hassan Saidy, alisema mradi wa kupeleka umeme kwenye vitongoji utahusisha makandarasi 25 ikiwa na thamani ya Sh. bilioni 363 kwa kila jimbo kupata vitongoji 15 isipokuwa kwa majimbo ya Mkoa wa Dar es Salaam.

Alisema mradi huo utatekelezwa kwa miezi 24 na hakutakuwa na kuongeza muda na kuhakikisha wanawashirikisha viongozi wa ngazi zote hatua ambavyo itaondoa migogoro.

Aliwataka makandarasi kuhakikisha vifaa vinashushwa kwenye vitongoji na kusisitiza kuwashirikisha wananchi pale wanapokata miti yao.

Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini, David Mathayo, alisema kamati inatoa rai kwa serikali kupitia Wizara ya Nishati kuhakikisha miradi hiyo inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyokubaliwa. 

Pia kuhakikisha miradi mingine inaendelea kutekelezwa na vitongoji vyote vinafikiwa na wananchi wananufaika na uwekezaji huo.