Zitto: Watanzania wamechoshwa na mauaji

By Halfani Chusi , Nipashe
Published at 06:42 PM Sep 12 2024
Kiongozi Mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo  Zitto Kabwe.
Picha: Mtandao
Kiongozi Mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe.

KIONGOZI Mstaafu wa Chama cha ACT Wazalendo Zitto Kabwe, amesema Watanzania wamechoshwa na mauaji yanayohusisha vyombo vya dola na wanapaswa kupata majibu ya uhakika ya nani yupo nyuma ya mauaji hayo.

"Ukimya wa wananchi usichukuliwe kuwa wamezoea matukio hayo kwa kuwa wakiamua kutoa sauti katika vifua vyao nchi haitotulia" amesema Zitto 

"Kazi ya Polisi ni kulinda haki za wote leo ACT haiko madarakani kesho itakuwa madarakani  hizi tabia za kutekana ni za hovyo, za kishamba na kikatili na haya mambo chama chetu kinayalaani kabisa" amesema Zitto

Akizungumza katika mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mbagala Zakheim, mkoani Dar es Salaam katika muendelezo wa ziara ya awamu ya pili, Mwenyekiti wa Chama hicho bara Isihaka Mchinjita, amesema ni ngumu kuamini katika uimara wa vyombo vya Ulinzi na Usalama nchini, akatokea mtu nje ya vyombo hivyo akawa na uwezo wa kumteka mtu hadharani bila ya kupata upinzani.

“Kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama kutaka watu wakatoe taarifa juu ya utekaji unaoendelea nchini, inalenga kuhamisha jukumu lao la msingi la ulinzi na Usalama na tunafahamu haya yanafanyika kwa ajili ya kuwatia hofu wananchi juu ya kuikosoa serikali” amesema

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo Bara, Isihaka Mchinjita akisalimia na baadhi ya wananchi walioshiruki Katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Jana Mbagala. PICHA: HALFANI CHUSI
Mchinjita amesema chama chake kinataka Rais Samia Suluhu Hassan afanyie  kazi mapendekezo ya tume ya haki jinai ambaye mwenyekiti wake alikuwa Jaji Mkuu Mstaafu Othman Chande, iliyofanya uchunguzi wa mwendendo wa utendaji wa Jeshi la Polisi.

"Sawa ni wakati ambao hatutaki kuendelea kusubiri jeshi letu linatia wasiwasi juu ya kulinda raia wake" alisema huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho walikuwa wamefurika kumsikiliza

Amesema jambo la pili wanalolitaka urudishwe tena muswaada wa sheria bungeni ili kikafutwe  kifungu kinachowaruhusu Askari wa Usalama wa Taifa kukamata raia. 

Amesisitiza kwamba asipofanya hivyo chama chake kitazunguka nchi nzima kuwaambia wananchi kwamba  yeye ndio muasisi wa masuala ya utekaji na mauaji yanayotokea kwakuwa ndiye aliyesaini sheria hiyo.

Amesema jambo la tatu Rais Samia  amfukuze kazi Waziri wake wa Mambo ya Ndani Hamad  Masauni.

"Masauni ni msaidizi wa Rais,  Katika mazingira haya watu wanatekwa na wanao jitambulisha kama ni askari msaada pekee anaoweza kuufanya kwaajili ya masilahi ya nchi ni kujiuzuru na kama ameshindwa Rais amfukuze kazi kwa sababu ameshindwa kusimamia usalama wa raia na Mali zake.

"Pia amfukuze kazi Mkuu wa Jeshi la Polisi  (IGP), Camilius Wambura  kwa sababu naye ameshindwa kulinda usalama wetu,  na ikiwa hatofukuzwa tukishika dola hata akiwa masestaafu au amekufa tutamrejeshea uongozi wake na kumfukuza ili tufute rekodi ya kwamba tuliwahi kuwa na IGP ambaye alishuhudia mauaji na utekaji bila kuchukua hatua yoyote" ameahidi Mchinjita