Watuhumiwa mauaji ya mjasiriamali wasakwa

By Christina Haule , Nipashe
Published at 11:29 AM Sep 17 2024
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama.
Picha: Mtandao
Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama.

JESHI la Polisi mkoani hapa linaendesha msako ili kumkamata au kuwakamata waliohusika na tukio la mauaji ya Costa Clemence (22), mjasiriamali na mkazi wa Maseyu, mkoani hapa.

Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Morogoro, SACP Alex Mkama, mauaji hayo yamebainika Septemba 15, katika Kijiji cha Gwata wilayani Morogoro.

Kamanda Mkama alisema mwili wa marehemu ulikutwa kwenye eneo ambalo halina makazi ya watu huku mwili ukiwa umetelekezwa na pembeni yake kukiwa na pikipiki isiyokuwa na namba za usajili inayosadikiwa kuwa ni mali ya marehemu.

Aidha, kamanda alisema uchunguzi wa kidaktari unafanyika kutambua kuwa mwili huo ulipatwa na shida gani kabla ya kupatwa umauti.

Alisema Jeshi la Polisi linatoa wito kwa wakazi wanaoishi maeneo hayo na yeyote mwenye taarifa kuhusu tukio hilo kuiwasilisha kwa polisi au mamlaka yoyote anayoona inafaa ili ushahidi uwepo katika kuwakamata wahusika wa mauaji hayo.