Biteko kuweka jiwe la msingi mradi bwawa kuzalisha umeme

By Joyce Lameck , Nipashe
Published at 08:43 PM Sep 18 2024
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko,
Picha:Mpigapicha Wetu
NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko,

NAIBU Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dk. Doto Biteko, kesho anatarajia kuwa mgeni rasmi katika hafla ya uwekaji jiwe la msingi mradi wa ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme katika Mto Malagarasi, mkoani Kigoma.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Mkuu Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Neema Mbuja, kukamilika kwa bwawa hilo kutawezesha kuzalishwa umeme wa megawati 49.5. Mradi utagharimu Dola za Marekani milioni 144.14 (Sh. bilioni 388).

Amesema kuwa kati ya fedha hizo, Serikali ya Tanzania itagharamia Dola za Marekani milioni 4.14 na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) itagharamia Dola za Marekani milioni 140 kama mkopo wenye masharti nafuu.

Neema amesema mradi huo pia utakuwa na uwezo wa kusafirisha umeme wa kilovoti 132 kutoka Igamba hadi Kidahwe (Km 54) na kituo cha kupoza, kusambaza umeme cha Kidahwe, mkoani Kigoma.

Vilevile, amesema mradi huo utahusisha sehemu kuu tatu; ujenzi wa bwawa la kuzalisha umeme likiwamo tuta, njia ya kupisha maji, nyumba ya kufua umeme yenye uwezo wa kuzalisha megawati 49.5 pamoja na kituo cha kupokea umeme.

Amesema sehemu ya pili itahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 132 (Km 54) ambayo itaunganisha kituo cha kuzalisha umeme na Gridi ya Taifa kupitia kituo cha kupoza umeme cha Kidahwe.

Amesema sehemu ya tatu ya mradi huo itahusisha ujenzi wa mtambo wa usambazaji umeme katika vijiji saba, ambavyo vinapitiwa na mradi huo ambavyo ni Mazungwe, Kidahwe, Kalenge, Kazuramimba, Mlela na Igamba.

Amesema umeme utakaozalishwa na mradi huo utasaidia mahitaji ya ndani ya Mkoa wa Kigoma pamoja na kuwezesha biashara ya umeme, huduma za kijamii, ikiwamo elimu, afya, maji pamoja na biashara za viwanda.